Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 19:42

Tunisia: Mivutano na wahamiaji katika mji wa Sfax yageuka ghasia


Vijana wa Tunisia wafunga barabara ya wahamiaji kwa kuchoma moto matairi huko Sfax. Picha na shirika la habari la AFP
Vijana wa Tunisia wafunga barabara ya wahamiaji kwa kuchoma moto matairi huko Sfax. Picha na shirika la habari la AFP

Mivutano ya rangi katika mji wa pwani wa Sfax nchini Tunisia imegeuka ghasia ikiwalenga wahamiaji kutoka barani Afrika chini ya jangwa la Sahara. Dazeni ya wahamiaji hao wameondolewa kwa nguvu kutoka mjini humo au kukimbia, walioshuhudia walisema Jumatano.

Huku kukiwa na vurugu Jumanne jioni, polisi waliwatia ndani baadhi ya wahamiaji na kuwapeleka hadi kwenye mpaka wa Libya zaidi ya kilometa 300 kutoka Safx, kwa mujibu wa kundi la ndani la kutetea haki.

Ghasia za karibuni zilianza baada ya mazishi ya mwanamme mmoja raia wa Tunisia mwenye umri wa miaka 41 ambaye alipigwa kisu na kufariki siku ya Jumatatu katika ugomvi baina ya wenyeji na wahamiaji, ambao ulipelekea kukamatwa kwa washukiwa watatu raia wa Cameroon.

Jonathan Tchamou, mwanafunzi raia wa Congo anasema, “Kuna tatizo kubwa sana huko Sfax. Mwananchi kutoka chini ya jangwa la Sahara alimuua mtunisia. Watunisia wamekasirishwa na wahamiaji wote. Watu nchini Tunisia wanawashambulia wahamiaji kutoka chini ya jangwa la Sahara na hata polisi wanajaribu kinyume cha sheria kuwakamata wahamiaji wa kiafrika na kuwarejesha kwenye eneo la jangwani huko Libya. Hili si jambo la kawaida. Kwa kweli tuna khofu kuwa hapa na ndiyo maana tunataka kuondoka Sfax kwa gharama yoyote ile.”

Sfax, mji wa pili kwa ukubwa katika taifa hilo la Afrika Kaskazini, ni sehemu ya kuondokea kwa wahamiaji wengi wenye matumaini ya kufika Italy mwanachama wa EU kwa kusafiri kwa njia ya bahari, kwenda kisiwa cha Lampedusa ambacho kiko umbali wa kilometa 130.

Mamia ya wakazi wenye ghadhabu walijaa katika mitaa ya Sfax Jumanne jioni wakidai kuondolewa kwa wahamiaj wote walioko kinyume cha sheria, alisema mwandishi wa AFP. Baadhi wameziba mitaa na kuchoma matairi ya gari.

Wahamiaji wakiwa Sfax. Julai 5 2023.
Wahamiaji wakiwa Sfax. Julai 5 2023.

Kanda za video kwenye mitandao ya kijamii ziliwaonyesha polisi wakiwafukuza dazeni ya wahamiaji kutoka kwenye nyumba zao huku wakishangiliwa na wakazi wa mjini humo, kabla ya kujaza kwenye magari ya polisi.

Mwanafunzi wa Congo Jonathan Tchamou anaelezea tena,“Tunisia ilikuwa nchi iliyotukaribisha. Tulikuwa hatuna wasi wasi hapa, lakini sasa hatukaribishwi tena nchini Tunisia, suluhisho litakuwa ni kuvuka Mediterranean kwenda Ulaya, kwasababu kurejea nyumbani kwetu si rahisi.”

Kwenye ukurasa wa Facebook wa kundi la kijamii la Sayeb Trottoir, mfanyakazi wa afya Lazhar Neji, akifanya kazi kwenye chumba cha dharura katika hospitali ya mjini humo, amesikitishwa na “umwagaji damu usio wa kibinadamu ambao unakufanya utetemeke ukiuangalia.”

Amesema hospitali ilipokwa kati ya wahamiaji 30 na 40 ambao wamejeruhiwa, wakiwemo wanawake na watoto, na kusema “baadhi walikuwa wamerushwa kutoka ghorofani, wengine wakishambuliwa kwa mapanga.”

Maafisa nchini Tunisia Jumanne waliwafukuza “wahamiaji 100” kutoka Sfax kuelekea kwenye mpaka wa Libya, wakisema katika taarifa ya pamoja iliyotolewa na Tunisia Forum for Economic and Social Rights (FTDES) na zaidi ya taasisi 20 zisizo za kiserikali.

“Kundi hilo lilijumuiah watu kutoka mataifa mbali mbali…. Wakiwemo takriban watoto 12 walio na umri kati ya miezi sita na miaka mitano,” iliongezea taarifa.

Baadhi ya wale waliondolewa kutoka Sfax “walipigwa”, taarifa ilisema.

Mwezi uliopita, mamia ya wakazi wa Sfax walipinga dhidi ya uwepo wa maelfu ya wahamiaji na kuitaka mamlaka kuwafukuza, wakisema Sfax hautakiwi kuwa mji wa wakimbizi.

Zied Mallouli, muandaaji wa maandamano anasema, “Leo, tuliandaa maandamano haya kwa hiyari kutokana na hali ya mivutano katika vitongoji na harakati za kihalifu, baadhi ambayo yalihusu kutumia mapanga. Tunaomba kusitishwa haraka kuwasili kwa wahamiaji haramu. Hatukuwa na matatizo hapo zamani, lakini leo matatizo yanatokea kwasababu yanatishia amani na usalama katika maeneo haya.”

Tunisia imeshuhduia ongezeko la mashambulizi yatokanayo na rangi ya mtu kufuatia maoni ya Rais Kais Saied mwezi Februari alipowashutumu wahamiaji haramu kwa kuleta ghasia na kutuhumu kwa njama wa kihalifu ili kubadili demografia ya nchi.

Huku ikiwa na idadi ya watu milioni 12, Tunisia inakadiriwa ni mwenyeji wa wahamiaji 21,000 kutoka sehemu nyingine za Afrika, wakiwakilisha asilimia 0.2 ya idadi ya watu.

Forum

XS
SM
MD
LG