Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 10:08

Trump na Biden watupiana shutuma kali katika mdahalo wao wa kwanza


Wagombea urais Donald Trump na Joe Biden
Wagombea urais Donald Trump na Joe Biden

Rais Donald Trump na Makamu wa Rais wa zamani, Joe Biden walijikita katika kuelezea sera na kutupiana shutuma kali katika mdahalo wao wa kwanza Jumanne usiku, wiki tano tu kabla ya uchaguzi wa rais.

Mdahalo ambao ulianza kawaida, haraka sana uligeuka ni malumbano ya kutupiana maneno juu ya masuala kadhaa ikiwemo COVID-19, ambayo mpaka hivi sasa watu karibu milioni moja kote ulimwenguni wamefariki na Marekani inaongoza kwa vifo 200,000.

Joe Biden : "Rais hana mpango. Hajaelezea chochote. Alifahamu muda mrefu tangu Februari jinsi mzozo ulivyo mkubwa.”

Trump alijibu kwa kusema majibu yake kwa janga hili yalikuwa na mafanikio akisema : “Tulipata nguo za kujikinga, tulipata barakoa, tulipata vifaa vya kusaidia kupumua. Wewe usingeweza kutengeneza vifaa vya kupumulia. Na hivi sasa tuko wiki chache tu kupata chanjo.”

Rais Donald Trump
Rais Donald Trump

Biden alishambulia juhudi za Trump kutaka kufuta Sheria ya Huduma Nafuu za Afya inayojulikana kama Obamacare, ambayo inatoa bima ya huduma za afya kwa kiasi cha watu milioni 20.

Trump amesema sheria hiyo ilikuwa kinyume cha katiba na inaweka viwango maalum kwa mteja. Biden amesema wanaweza kuendelea na mipango yao binafsi ya afya kulingana na pendekezo la kupanua Obamacare.

Biden alifafanua : “Wanaweza kufanya hivyo, na wanaweza kwa mujibu wa pendekezo langu.”

Haraka mambo yalibadilika wakati kila mmoja alizungumza juu ya mwenzake.

Naye Rais Trump alisema :"Obamacare si nzuri. Sisi tuna mpango mzuri zaidi."
Trump amemshutumu Biden kwa kufuta afya ya kijamii.

Jambo jingine ambalo lilikuwa na ubishani mkali: Uteuzi wa Trump kujaza nafasi katika mahakama ya juu Marekani ambayo imeachwa wazi kutokana na kifo cha Jaji mliberali Ruth Bader Ginsburg.

Trump amemteua Jaji mconservative Amy Coney Barrett, na kuanzisha mchakato wa kuthibitisha wakati upigaji tayari umeanza katika majimbo mengi.

Biden anasema yeyote ambaye atashindwa uchaguzi wa mwezi November ni vyema ndiyo ajaze nafasi ya Ginsburg.

Makamu wa Rais Joe Biden
Makamu wa Rais Joe Biden

Biden : “Wamarekani wana haki ya kusema nani awe mteuliwa wa mahakama ya juu.”

Trump alijibu kwamba ni wajibu wake kutaja atakayejaza nafasi hiyo bila ya kujali muda.

“Tumeshinda uchaguzi na hivyo tuna haki ya kumchagua,” amesema Rais Trump.

Afisa katika kampeni ya Trump, Tim Murtaugh, anasema ameridhishwa na mdahalo ulivyokwenda.

“Watazamaji walichokiona ni kwamba Rais Trump alikuwa akiongoza kila wakati katika mdahalo huo nadhani wameona mara nyingi udhaifu wa Joe Biden, alitumia muda mwingi kutazama apewe msaada na muongoza mdahalo huo.”

Wachambuzi wanasema ulikuwa ni mdahalo kila mmoja akifanya lake.

Jeremy Mayer wa Chuo Kikuu cha George Mason : “Na pale Biden alipozungumza, mara nyingi alikuwa akitoa pointi nzuri kwa sekunde 10, 20, 30 na ghafla ataingiliwa kati, kila mara na rais. Kwahiyo kuuliza nani kashinda mdahalo huu hakuna maana kwasababu Rais kwa hakika alihakikisha kuwa hakuna mdahalo wa rais.”

Duru ya kwanza imemalizika, midahalo mingine miwili inatarajiwa kufanyika mwezi huu.

XS
SM
MD
LG