Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 16:31

Wamarekani waendelea kutoa heshima zao za mwisho kwa mwili wa hayati Jaji Ginsburg


Rais Donald Trump na mkewe Melania Trump wakitoa heshima zao kwa mwili wa hayati Ruth Bader Ginsburg uliowekwa jengo la Mahakama ya Juu Sept. 24, 2020, mjini Washington.
Rais Donald Trump na mkewe Melania Trump wakitoa heshima zao kwa mwili wa hayati Ruth Bader Ginsburg uliowekwa jengo la Mahakama ya Juu Sept. 24, 2020, mjini Washington.

Maefu ya Wamarekani kutoka sehemu mbali mbali za nchi wamekuwa wakitoa heshima zao za mwisho kwa Jaji mashuhuri wa Mahakama ya Juu mtetea haki za wanawake na usawa wa jinsia Ruth Bader Ginsburg mbele ya jengo la mahakama hiyo tangu Jumatano mchana.

Kifo cha Jaji huyo kimeacha nafasi muhimu katika mahakama yenye viti 9, inayozusha mjadala mkubwa kote nchini na kumpatia nafasi rais Donald Trump kumteua jaji wa tatu wa mahakama hiyo akiwa madarakani.

Hii ni wiki ya huzuni na mvutano mkubwa kutokana na kifo hicho cha Ginsburg ambaye mwili wake umewekwa mbele ya jengo hili kwa watu kutoa heshima zao za mwisho kabla ya kupelekwa katika jengo la bunge kuagwa rasmi kitaifa.

Atakua ni mwanamke wa kwanza ambaye mwili wake utawekwa katika ukumbi mkubwa wa bunge ili wabunge na taifa zima kumuaga shujaa wa taifa wa kutetea masuala muhimu ya kijamii na wanawake hapa nchini.

Kifo cha hayati Ginsburg kimegubikwa na hali ya kisiasa pale rais Trump alipotangaza atamtaja mtu atakaye chukua nafasi yake siku ya Jumamosi.

Rais Donald Trump
Rais Donald Trump

Jambo linalozusha mjadala mkali wa itikadi kati ya Wademokrats na Warepublican bungeni na kati ya wananchi wenye kufuata siasa za mrengo wa kulia wanaotaka utaratibu wa kumteua mtu uendele na wale wa mrengo wa kushoto wanaotaka utaratibu usitishwe hadi baada ya uchaguzi wa novemba 3.

Watu wanaofika hapa kutoa heshima zao za mwisho wanasema lengo lao kubwa ni kukumbuka mchango wake katika maisha ya Wamarekani.

Rais Trump akifuatana na mkewe Melania alikuwa miongoni mwa watu waliokuja hapa mapema kutoka heshima zake.

Rais mstaafu Barack Obama
Rais mstaafu Barack Obama

Marais wa zamani Bill Clinton na Barack Obama wakifuatana na wake zao walitoa heshima zao hapo Jumatano pamoja na wanasiasa maarufu wengi wa Marekani.

Rais mstaafu Bill Clinton
Rais mstaafu Bill Clinton

Hii leo wachambuzi wanasema kifo chake hivi sasa kimebadili muelekeo wa kampeni za uchaguzi mkuu, na kuweka nyuma masuala ya uchumi, janga la corona na ajira.

Akiwa katika moja ya kampeni zake mjini Swanton Ohio wiki hii Rais Trump, aliwaambia wafuasi wake kwamba wakati taifa linaomboleza kifo cha Ginsburg yeye atamtangaza mtu atakaye chukua nafasi yake karibuni.

Donald Trump alieleza : "Ikiwa Joe Biden na wademokrats watachukua madaraka wataijaza mahakama kuu na wafuasi wa itikadi kali za mrengo wa kushoto ambao wataigeuza kabisa jamii ya Marekani hata hatutoweza kuitambua tena. Basi huenda nikamteua mtu Jumamosi ambaye mtampenda, mtamheshimu."

Makamu wa Rais wa zamani Joe Biden
Makamu wa Rais wa zamani Joe Biden

Wademokrat wakiongozwa na mgombea wao wa kiti cha Rais Joe Biden wanataka utaratibu usubiri hadi baada ya uchaguzi wa Novemba 3. Kiongozi wa walio wachache katika baraza la Seneti Chuck Schumer aliwakosoa wenzake wa Republican kwa kuwa wanafiki waliobadili msimamo wao baada ya kudai miaka minne iliyopita kwamba sio jambo la busara kumteua jaji wa mahakama ya juu mnamo mwaka wa uchaguzi pale rais wa zamani alipotaka kumteua jaji kuchukua nafasi ya Antony Scalia miezi minane kabla ya uchaguzi.

Schumer ameeleza : "Hatua za kiongozi McConnell huenda zikavuruga kabisa chombo cha senate. Ikiwa McConnell ataendelea na utaratibu, Warepublican waliowengi watakuwa wameiba viti viwili vya mahakama kuu katika kipindi cha miaka minne kwa kutumia hoja zinazokinzana kabisa.

Maombolezi yataendelea Alhamisi na Ijumaa kuomboleza kifo cha hayati Ginsburg na kuenzi juhudi zake za kuleta mabadiliko wakiacha kando mvutano wa kisiasa ambao utaanza kwa nguvu wiki ijayo hasa baada ya kuzikwa kwenye makaburi ya Arlington wanakozikwa wanajeshi na maafisa wakuu wa serikali.

XS
SM
MD
LG