Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Novemba 06, 2024 Local time: 04:50

Trump na Biden wanajiandaa kwa mdahalo wa kwanza Jumanne


Rais Donald Trump (kulia) na Makamu wa Rais wa zamani Joe Biden
Rais Donald Trump (kulia) na Makamu wa Rais wa zamani Joe Biden

Uchaguzi wenye ushindani mkali hapa Marekani unaingia katika awamu muhimu wiki hii pale Donald Trump na Joe Biden watakapokutana kwa mdahalo wa kwanza Jumanne, ambao hatimaye utawapatia wapiga kura fursa ya kufahamu misimamo tofauti iliyopo kati ya wagombea hao wawili.

Mdahalo huu unafanyika muda mfupi tu baada ya Trump kukaidi ombi la Wademokrats la kutomteua mtu kuchukua nafasi ya Jaji wa mrengo wa kushoto hayati Ruth Bader Ginsberg, kwa kumteua

Jaji Amy Coney Barrett
Jaji Amy Coney Barrett


wa mrengo wa kulia katika mahakama ya juu.

Zikiwa zimebaki siku 35 za kampeni kali za uchaguzi mkuu hapa Marekani, inaonekana suala la uteuzi wa jaji wa Mahakama ya Juu linachukuwa nafasi ya juu hivi sasa.

Jaji Barrett ataanza kukutana na viongozi wa baraza la Seneti wiki hii kabla ya kuanza kwa vikao vya kumthibitisha kuwa jaji katika mahakama hiyo - ikiwa ni uteuzi wa maisha inayoweza kuleta mabadiliko makubwa katika sheria na maisha ya Wamarekani. Warepublican wanaonekana wako tayari na utaratibu na wanakura zinazohitajika kumthibitisha.

Na rais Trump anasema ni muhimu kwa mahakama hiyo ya majaji 9 iwe imekamilika kwani watahitajika kuamua juu ya matokeo ya uchaguzi wa Novemba 3 ikiwa kuna malalamiko.

Rais Trump asema : "Ninadhani ni bora ikiwa itafanyika kabla ya uchaguzi kwa sababu ninadhani hii njama ambayo Wademokrats wanapanga, ni njama itakayofikishwa mbele ya mahakama ya juu ya marekani na ninadhani kuwepo na majaji wanne upande wa kulia na wanne upande wa kushoto hali haitokuwa nzuri.

Rais Donald Trump
Rais Donald Trump

Trump amekuwa akidai - bila ya kutoa ushahidi- kwamba kutakuwepo na wizi wa kura kutokana na watu kupiga kura kupitia posta. Na ikiwa Warepublican watabisha matokeo ya uchaguzi kesi huenda ikafikishwa mbele ya mahakama ya juu ambako kura ya Jaji Barrett itakuwa muhimu pale kura zitakapokuwa sawa nne kwa nne.

Ukusanyaji wa maoni wa hivi karibuni uliofanywa na New York Times na chuo cha Sienna, unaonyesha asilimia 56 ya Wamarekani wanapendelea rais ajae ndiye amchague jaji mpya.

Joe Biden mgombea kiti cha urais kwa niaba ya chama cha Demokratik Jumapili aliwataka wa Republican kuruhusu wapiga kura wamchague rais kwanza kabla ya kumthibitisha jaji mpya.

Makamu wa Rais wa zamani Joe Biden
Makamu wa Rais wa zamani Joe Biden

Makamu wa Rais wa zamani Biden anasema : "Kwa vile tu una madaraka kufanya kitu, haimanishi unaweza kuacha jukumu lenu la kuwafanyia Wamarekani jambo lililo sahihi."

Hivi sasa wagombea hao wawili wanajitayarisha kwa mdahalo wao wa kwanza kati ya midahalo mitatu, ambapo suala hilo la uteuzi wa jaji litachukua nafasi muhimu. Lakini Trump atakabiliwa hasa na changamoto ya kujibu namna alivyokabiliana na janga la virusi vya corona vilivyosababisha zaidi ya vifo laki mbili hapa Marekani.

Mnamo kipindi hichi cha kampeni Biden amekuwa akibaki karibu na jimbo lake la Delaware akichukuwa tahadhari dhidi ya janga hilo wakati rais akitumia ndege yake ya Airforce One akifanya mikutano ya hadhara akikaidi muongozo wa waatalamu wake wa afya.

Msimamizi wa mdahalo Chris Wallace amepanga masuala kuanzia kuporomoka kwa uchumi, kupunguka sana ajira, ubaguzi wa rangi na uhalali wa uchaguzi wenyewe. Kilichobaki ni kuona jinsi wagombea hao wawili watakavyo parurana.

XS
SM
MD
LG