Jumamosi jioni Mkuu wa Wafanyakazi wa White House Mark Meadows amekiambia kipindi “Justice with Jeannine” cha kituo cha televisheni cha Fox News kulikuwa na wasiwasi juu ya hali ya rais Ijumaa.
“Jana tulikuwa na wasiwasi kwelikweli,” Meadows amesema. Yeye (Trump) alikuwa na homa na kiwango cha hewa ya Oxygen katika damu yake kilishuka sana.”
Mapema leo, jopo la madaktari wanaomtibu rais wametoa ripoti yenye matumaini.
“Leo asubuhi rais anaendelea vizuri,” Sean Conley, amewaambia waandishi wa habari Jumamosi asubuhi kwenye Kituo cha Tiba cha Kijeshi cha Taifa cha Walter Reed.
Katika taarifa mpya ya Jumamosi usiku, amesema Trump amepewa dozi ya pili ya remdesivir, “ hana homa na hatumii hewa ya oxygen ya ziada anapumua vizuri kwa asilimia 96 hadi 98 siku nzima.
Wakati rais hajatoka katika hatari ya ugonjwa, madaktari wake wanachukuwa tahadhari wakiwa na matumaini, taarifa ya Conley imesema.
Trump ataendelea kupewa dozi zaidi ya dawa ya Remdesiver Jumapili, na madaktari wake wataendelea kufuatilia kwa karibu sana hali yake, taarifa imesema.