Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 25, 2024 Local time: 19:54

Tanzania : Magufuli atangaza siku 3 za maombolezo ya kitaifa


Rais John Pombe Magufuli
Rais John Pombe Magufuli

Rais John Magufuli ametangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kuanzia Jumamosi na kuwa serikali itagharamia matibabu ya majeruhi wa ajali ya lori lililolipuka na kuua zaidi ya watu 60 mkoani Morogoro Jumamosi.

Rais amesema serikali itagharamia matibabu ya majeruhi wa ajali ya lori lililolipuka na kuwa moto mkoani Morogoro jana Jumamosi Agosti 10.

Wakati huohuo Rais amemtuma Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa kumwakilisha katika mazishi ya marehemu wa ajali hiyo yanayotarajiwa kufanyika Jumapili.

Kadhalika Rais Magufuli amewataka Watanzania kutokuwa majaji na wepesi wa kuhukumu bila kufahamu chanzo cha ajali hiyo.

Vyanzo vya habari nchini humo vimeripoti Rais Magufuli amesema hayo leo Jumapili Agosti 11, wakati alipowatembelea baadhi ya majeruhi waliolazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

“Niwaombe Watanzania tuendelee kuwaombea huu si wakati wa kulaumu kwa sababu nimesikia wengine wanasema walikuwa wameenda kuiba mafuta.

“Tusihukumu bila kufahamu chanzo kwa sababu kuna mmoja amesema alikuwa kwenye lori jingine alivyoona ajali akashuka ili akatoe msaada lakini aliungua, kwa hiyo si wote walikwenda kuiba mafuta wengine walikwenda kutoa msaada.

“Yupo mwingine alikuwa anasema anasafiri kwenda Mtwara wakazuiwa, akaungua. Sisi tusiwe majaji kwa sababu si kila mmoja alikuwa anakwenda kuiba mafuta wengine walikuwa wanapita njia tu,” amesema Rais Magufuli.

Aidha, akiwa hospitalini hapo Rais Magufuli alipokea taarifa kuwa majeruhi waliofikishwa Muhimbili walikuwa 46 ambapo watatu kati yao wamefariki huku wengine 15 wakiendelea na matibabu mkoani Morogoro.

Rais Magufuli pia amewashukuru madaktari na wauguzi hospitalini hapo kwa kuwahudumia wagonjwa hao kwa njia mbalimbali na kuokoa maisha yao ambao wengi wao wameungua vibaya.

“Muhimbili imebadilika sana huduma ni nzuri najua mna changamoto nyingi sana serikali tunatakiwa kuzitatua lakini tunaomba mjitahidi hivyo hivyo,” amesema.

Akiwa hospitalini hapo, Rais Magufuli amewatembelea majeruhi hao na kuwapatia Sh 500,000 kila mmoja na madaktari na wauguzi wanaowahudumia wagonjwa hao.

XS
SM
MD
LG