Baada ya wimbi la ghasia za waasi kumuharibia tena maisha yake, Buregeya na familia yake waliukimbia mji wa Kibumba mwezi Oktoba wakati mashambulizi mapya ya kundi la waasi la M23 yalipoanza – kwa mara ya tatu katika kipindi cha miaka 15 amelazimika kukimbia nyumbani kwake na ameshindwa kusoma kwa kipindi cha mwaka mzima. Sasa ana umri wa miaka 22 na bado anasubiri kumaliza shule.
"Nikiwa hapa kambini ninapoona ... wahitimu kama mimi, moyo unaniuma, najiuliza ni lini nitamaliza masomo yangu, miaka inapita," alisema.
Katika kambi ndogo iliyoko karibu na kanisa la kiinjili, nje ya mji mkuu wa mkoa Goma, Buregeya anatumia muda wake kujiegemeza katika ukuta wa bati wa kanisa au kucheza karata na marafiki zake kutoka shule ambao pia walihamia kambini wakitokea Kibumba.
Buregeya anapatwa na hofu anapoona siku zinapozidi kusonga. "Ndoto yangu ya maisha ilikuwa kwenda chuo kikuu baada ya masomo ya sekondari, na kutafuta kazi, kuwa mwalimu na kujikimu kimaisha,” alisema.
Yeye ni mmoja wa vijana 750,000 wa Congo ambao masomo yao kwa sasa yamekatishwa kutokana na ukosefu wa usalama katika mikoa iliyoko mashariki mwa Kivu Kaskazini na Ituri, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF) lilikadiria mwishoni mwa mwezi Machi.
Tangu mwezi Januari 2022, shule zipatazo 2,100 zilizoko mashariki mwa Congo zimefungwa kwasababu ya vita, kulingana na UNICEF.