Kwa siku za hivi karibuni nchi hiyo imegonga vichwa vya habari kutokana na sakata la wakimbizi na watafuta hifadhi kutoka Uingereza kupelekwa Rwanda lakini pia sintofahamu kati yake na shirika la kutetea haki za wakimbizi, UNHCR.
Zaidi ya wakimbizi 136, 00 wanapatikana katika kambi mbalimbali za wakimbizi nchini Rwanda, wengi wao wanaishi nchii kwa takribani miongo mitatu sasa, hawana wanatokea katika nchi jirani za Burundi na Jamhuri ya Kidmokrasia ya Kongo. Walikimbia machafuko nchini mwao na kupewa hifadhi nchini Rwanda ambayo nayo wakati Fulani wake ama waliwahi kuwa wakimbizi au walizaliwa ukimbizini.
Moja ya kambi kubwa za wakimbizi hawa ni ile ya Mahama mashariki mwa Rwanda ambako kunahifadhiwa zaidi wakimbizi elfu 71 kutoka Burundi na DRC
Katika kambi moja, wakimbizi wanaainisha changamoto zinazowakabili.
"Kama unavyoshuhudia hatuna nishati ya kupikia, hakuna kuni wala chochote cha kutumia kupikia chakula tunachokipata, unapambana kupata chakula lakini ukikipata changamoto inakuwa sasa ni ya kupata kuni za kupikia, ni shida tupu," mmoja wao anasema.
"Hali ikiendelea hivi tutapata taabu zaidi, maana hatuna uwezo," mwingine anasema.
Shirika la umoja wa mataifa la huduma kwa wakimbizi na serikali ya Rwanda kama mdau siku zote wamekuwa wakisema mkimbizi ana haki ya kuishi salama na pia ana hakoi ya kurudi nyumbani kwa hiari bila shurutu
Mwaka jana baadhi ya wakimbizi wa Burundi walirejea nyumbani lakini baadaye mchakato huu ulisimama kwa kile kilichodaiwa na baadhi ya wakimbizi kuwa hali haikuwa salama kwa baadhi ya wale waliorejea kwao.
"Kuna waliorejea nyumbani na baadaye kutoroka tena kurudi kutokana na usalama, kwa kuwa kuba hata baadhi waliouawa baada ya kufika kule yaani ni shida," anasema mmoja wa wakimbizi.
Haya yanatokea miezi michache baada ya shirika la umoja wa mataifa la huduma kwa wakimbizi kutangaza azma yake ya kupunguza kiasi cha misaada kwa wakimbizi waishio Rwanda kutokana na kupungua kwa misaada
Wakati haya yote yakiarifiwa serikali ya Rwanda kwa upande mwingine imekuwa siku zote ikisema kwamba inafanya kila jitihada kuhakikisha maisha ya wakimbizi waishio Rwanda bila kujali nchi wanakotoka wanaishi kwa amani na usalama meja Jenerali mstaafu Albert Murasira ni waziri anayehusika na huduma kwa wakimbizi
Mej Gen(Rtd) Albert Murasira anasema: "Ninaweza kusema kwamba mkimbizi yeyote aliyeko hapa ana haki sawa na mzalendo wa nchi hii, tofauti tu ni kuwa mtu huyu hayuko katika nchi yake asilia lakini pia akiwa hapa haruhusiwi kujihusisha na masuala ya kisiasa, laini mambo mengine yuko maana hatumzuii kutoka kambini, wala hatumtaki aombe idhini ya kwenda uraia pengine tunachomuomba ni kutujulisha kule anakoenda ili akipata tatizo tujue jinsi ya kumsaidia, vinginevyo kila mkimbizi ana haki ya usalama, uhuru wa kutembea kufanya shughuli za kujikimu nje ya kambi na mambo mengine ya msingi."
Wakati dunia ikiadhimisha siku ya wakimbizi kwa upande mwingine kunaendelea sakata la kuwahamishia nchini Rwanda wakimbizi na watafuta hifadhi kutoka Uingereza kwenda Rwanda, sakata hili ambalo limekuwa mahakamani na katika vyombo vya dola kule Uingereza vimeifanya Rwanda na Uingereza kugongwa vichwa vya habari kila mara. Hata hivyo serikali za nchi mbili mara zote zimetangaza utayari wake wa kuwahamisha na kuwapokea wakimbizi hao nchini Rwanda lakini wanasheria na watetezi wa haki za binadamu wanaendelea kulippinga hilo,
Kwa upande mwingine lakini Rwanda hadi sasa inaendelea kuwapokea watafuta hifadhi wengine kutoka Libya ambapo zaidi ya elfu 15 wameshaingia Rwanda,
Mayardt Shilo anatoka Sudan Kusini lakini aliingia Rwanda akitokea Libya.
"Nilikimbia kutoka Sudan Kusini kutokana na matatizo ya kivita, kubakwa, kuuawa na kadhalika na baadaye nikakimbilia Libya nikijua nitavuka kwenda ulaya lakini nikiwa kule hali ilikuwa ambaya zaidi kuliko hata nilikotoka nyumbani, Libya ni kubaya mno, ni mahali hatari sana, sasa niko hapa naajihisi niko salama," anasema.
Kupitia michakato hii yote Serikali ya Rwanda na shirika la kutetea haki za wakimbizi wamekuwa na ushirikiano wa karibu. Lakini wiki iliyopita pande zilijikuta katika mzozo wa maneno baada ya UNHCR kuisuta Rwanda kushindwa kuwanyima haki ya kuwapokea baadhi ya wakimbizi ambao UNHCR haikutangaza uraia wao suala ambalo lilisababisha serikali ya Rwanda kukanusha vikali madai hayo ikiyataja kama ya uzushi mtupu
Mej Jen mstaafu Albert Murasira, waziri anayehusika na masuala ya wakimbizi.
"Wewe fikiria wanasema tulikataa kuwapokea watu kama saba hivi,na ukitathmini mienendo ya watu hao utakuwa ni watu ambao walinyimwa haki ya ukimbizi katika mataifa mengine, hivi itakuwaje tuwapokee watu zaidi laki moja na elfu thelathini na wakati huo tushutumiwe kushindwa kuwapokea watu saba tu, hivi huoni tatizo hapo, Mej Jen mstaafu Albert Murasira ansema.
Takwimu za hivi punde zaidi zinaonyesha kuwa wakimbizi elfu 84 ni wa kutoka DRC elfu 51 kutoka Burundi, elfu 15 kutoka Libya.
Forum