Mkuu wa Baraza la Usalama la Russia Nikolai Patrushev ameyalaumu majeshi ya Ukraine kwa kutekeleza shambulizi kwenye kinu cha nyuklia, akisema wanatumia “silaha za Magharibi ambazo zinaweza kupelekea kutokea janga kwa ulimwengu mzima.”
Tamko la Patrushev limekuja baada ya mkuu wa jeshi la Ukraine kusema awali kuwa mashambulizi ya Russia yalilenga eneo kubwa la nchi kwa mashambulizi ya makombora, kuharibu miundombinu na usambazaji wa nishati katika kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia, ambacho ni kikubwa kabisa Ulaya.
Kinu hicho kilichopo kusini mwa Ukraine kimezimwa, maafisa walisema, kina uharibifu kwenye njia za kusambaza umeme wa nguvu ya juu na kinategemea majenereta yanayotumia dizeli, kampuni ya kuzalisha umeme ya Ukraine, Energoatom ilisema.
“Adui huyu anajaribu kuendelea kuyakamata kwa muda maeneo aliyoyateka, akiongeza juhudi kuzuia hatua za majeshi ya ulinzi katika baadhi ya sehemu,” mkuu wa jeshi la Ukraine alisema Alhamisi.
Pande zote zinakanusha madai ya kila upande. Lakini, mapigano makali yameripotiwa katika mikoa ya mashariki ya Luhansk na Donetsk, kulingana na ripoti, na mashambulizi ya Russia yameripotiwa huko Kriviy Rih, katikati ma Ukraine, na huko Sumy na Kharkiv, upande wa kaskazini mashariki.
Siku ya Alhamisi, kikundi cha G7 cha nchi zinazofuata demokrasia zitakutana katika mji wa Muenster magharibi mwa Ujerumani kwa siku mbili kujadili njia bora ya kuratibu na kuendelea kutoa msaada kwa Ukraine. Mkutano huo unakuja huku mashambulizi mapya ya Russia yakielekezwa katika miundombinu ya nishati ikisababisha kukatika umeme kila mahali, kulingana na ripoti.
Baadhi ya taarifa hizi zinatokana na mashirika ya habari ya AP, AFP na Reuters.