Maafisa wa jeshi katika mji mkuu wa Libreville, waliwafungulia mashtaka wajumbe hao wiki hii kwa tuhuma za uhalifu, ikiwa pamoja na uhaini na ufisadi.
Maandamano yamekuwa yakifanyika katika miji kadhaa kuonyesha mshikamano na hatua za utawala wa kijeshi.
Mwendesha mashtaka wa serikali mjini Libreville, Andre-Patrick Roponat, alisoma majina na kukiambia kituo cha Televisheni ya Taifa ya Gabon kuwa watu wawili kati ya 12 waliokamatwa Agosti 30, muda mfupi baada ya jeshi la Gabon kuchukua madaraka kutoka kwa Ali Bongo, wataachiliwa huru.
Katika mazungumzo ya Jumatano jioni, mwendesha mashitaka alisema, watu watatu akiwemo Sylvia Bongo Ondimba, ambaye ni mke wa rais aliyeondolewa madarakani Ali Bongo, wamewekwa katika kizuizi cha nyumbani.
Serikali ya Gabon inamshutumu mke wa rais kwa kujaribu kuwalinda watu wanaohusika na uhalifu, lakini hajatoa maelezo yoyote.
Roponat alisema mtoto mkubwa wa Ali Bongo, Noureddin Bongo Valentin, msemaji wa zamani wa rais Jessye Ella Ekogha, na wasaidizi wengine watano wa karibu wa kiongozi aliyeondolewa madarakani wanazuiliwa kwa muda.
Roponat anasema washukiwa hao watajibu mashtaka yakiwemo ya kupanga ghasia na udanganyifu wakati wa uchaguzi, kughushi saini ya rais wa Gabon, rushwa, ubadhirifu, utakatishaji fedha, manunuzi haramu na kujilimbikizia mali, uhaini na uhalifu mwingine kadhaa.
Televisheni ya taifa ilionyesha video ya wanajeshi wa serikali wakipekua nyumba za mawaziri wa zamani na kukamata makasha, masanduku na mifuko iliyojaa fedha.
Utawala wa kijeshi haujaeleza bayana kiasi gani cha fedha ambacho wanaamini kilikuwa kikishikiliwa na maafisa hao wa zamani, lakini wizara ya sheria inasema fedha nyingi zilipatikana kutoka kwa mtoto mkubwa wa rais aliyeondolewa madarakani.
Kila mara upinzani wa kisiasa nchini Gabon umekuwa ukimshutumu Noureddin kwa kupanga kuchukua mamlaka kutoka kwa baba yake.
Ali Bongo aliingia madarakani mwaka 2009, kufuatia kifo cha baba yake, Omar, ambaye aliiongoza nchi hiyo iliyoko Afrika ya Kati tangu 1967.
Upinzani nchini Gabon, wanaharakati na mashirika ya kiraia wameandamana katika miji kadhaa, ikiwemo Libreville, Franceville na Port-Gentil wiki hii kuunga mkono ukamataji huo.
Forum