Ripoti hiyo iliyotolewa Jumapili na Iran inaonyesha abiria walikuwa bado hai kwa muda baada ya athari za mlipuko wa kwanza kutokea.
Tangazo hilo limetolewa na Touraj Dehghani-Zanganeh, mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Iran na ni hatua ya kwanza ya ripoti rasmi inayoeleza maudhui yaliyopatikana ya sauti za marubani na rikodi za takwimu, ambazo zilitumwa Ufaransa kusomwa mwezi Julai.
Tehran tayari imesema kwamba iliitungua ndege ya Ukraine kwa bahati mbaya mwezi Januari, wakati wa mvutano wa hali ya juu baina yake na Marekani. Abiria wote 176 waliuawa.
Dehghani-Zanganeh amenukuliwa na televisheni ya kitaifa akisema, “Sekunde 19 baada ya kombora la kwanza kupiga ndege hiyo, sauti za marubani ndani ya ndege, zinaonyesha kwamba abiria walikuwa bado hai … sekunde 25 baadae kombora la pili lilipiga ndege hiyo”
Iran imekuwa katika mazungumzo na Ukraine, Canada na nchi nyingine ambazo walikuwa na raia wao katika ndege hiyo iliyotunguliwa, na ambao wameshinikiza kuwepo uchunguzi wa kina juu ya ajali hiyo.
“Takwimu zilizochambuliwa kutoka katika black boxes zisitumiwe kisiasa,” Zanganeh amesema.
Jeshi la Kulinda Mapinduzi ya Iran, Revolutionary Guards walitungua ndege hiyo ya Ukraine iliyokuwa kwenye safari ya kimataifa, kwa kombora la kutoka ardhini kwenda angani Januari 8, mara baada ya ndege kuondoka Tehran.
Jambo ambalo baadae Tehran ilikubali kuwa ni “kosa la kusikitisha” lililofanywa na vikosi ambavyo vilikuwa katika hali ya juu ya tahadhari wakati wa mgogoro wake na Marekani.
Maafisa wa Iran na Ukraine wamekuwa wakifanya mazungumzo juu ya utaratibu wa fidia kwa familia za abiria waliouawa. Duru nyingine ya mazungumzo hayo imepangwa kufanyika Octoba 2020.