Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 26, 2024 Local time: 21:58

Mudavadi aandamwa na madai ya usaliti baada ya kutangaza ushirikiano na Ruto


Musalia Mudavadi
Musalia Mudavadi

Muungano wa kisiasa wa One Kenya Alliance nchini Kenya uliowaleta pamoja wanasiasa wa muda mrefu, ambao kwa mwongo mmoja sasa wamekuwa katika upinzani nchini humo, Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi, Moses Wetangula na Gideon Moi, uko katika hatari ya kusambaratika baada ya Musalia Mudavadi kutangaza ushirikiano na makamu wa rais wa nchi hiyo William Ruto.

Musalia Mudavadi, Makamu wa Rais wa zamani anaandamwa na madai ya usaliti kutoka kwa vinara wenzake, kwa kukaribisha usuhuba wa kisiasa na William Ruto ambaye wamekuwa wakimshambulia kwa maneno.

Makamu wa Rais William Ruto
Makamu wa Rais William Ruto

Muungano huo ulikuwa umependekeza Mudavadi kuwa mgombea mwenza wa Kalonzo Musyoka katika kura ya urais mwaka 2022.

Kitendo cha Mudavadi na Wetangula kinaonekana ni njama ya siri kuidhinisha ushirikiano wa kisiasa na naibu rais wa Kenya William Ruto, ambaye pia ametangaza azma yake ya kugombea urais, Agosti 9 mwaka 2022, kimeibua madai ya ulaghai na usaliti ndani ya Muungano wa One Kenya Alliance.

Waliokuwa vinara wenza wa Mudavadi, Kalonzo Musyoka wa Wiper Democratic, Gideon Moi wa KANU na Cyrus Jirongo wameripotiwa kugadhabishwa na hatua ya kiongozi huyo wa Amani National Congress kufikia makubaliano ya kushirikiana kisiasa na Ruto bila mashauriano katika muungano huo licha ya kuwapo mazungumzo ya kina kutangaza ugombea wake katika kura ya urais.

Vile vile, viongozi hao wamekasirishwa na kitendo cha Mudavadi kumkaribisha Ruto kuwa mgeni katika hafla yake ya kutangaza azma ya kuwania urais, Jumapili katika ukumbi wa Bomas jijini Nairobi bila kuwaarifu, kitendo kilichowafanya Musyoka na Moi kuondoka haraka katika ukumbi huo.

Hadi wakati huo, suala la Ruto kufanya kazi na Mudavadi lilikuwa limesalia kuwa uvumi hadi wanasiasa wanaomuunga mkono Ruto, baadhi wakiwa wamevalia mavazi yaliyokuwa na nembo ya ANC—chama cha Mudavadi na UDA—chama cha Ruto walipofika ukumbini hapo.,

Wabunge wanaomuunga mkono Kalonzo Musyoka katika chama cha Wiper Democratic wamemtaja Mudavadi kama msaliti na mtu asiyeaminika.

Jopo la kiufundi lililoundwa na One Kenya Alliance, katika mapendekezo yake ambayo bado hayajatangazwa kwa umma, liliafikiana Mudavadi kuwa mgombea mwenza wa Kalonzo Musyoka katika kura ya urais mwaka huu, kutokana na uwezo wa Musyoka kufikia wapiga kura wengi, uwezo wa kifedha kufadhili kampeni za kisiasa na kukubalika na makundi mengine yasioegemea popote.

Lakini wakati chama cha Ruto kikisema kinaanza msururu wa mikutano kutangaza ushirikiano na Mudavadi, mkuu wa vyama vya wafanyakazi nchini Kenya Francis Atwoli amemtaja Mudavadi kuwa muoga.

Mark Bichachi, mfuatiliaji wa siasa za Kenya anaeleza kuwa Musyoka na Moi wanajikuta kwenye njiapanda kisiasa baada ya hatua hiyo ya Mudavadi kujiunga na Ruto, licha ya kuwa nao katika muungao huo.

Jumatatu, wabunge wa chama cha Ruto wameidhinisha kwa kauli moja ushirikiano wake na Bw Mudavadi na chama chake, kupisha mikutano na kampeni za pamoja.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Kennedy Wandera, Nairobi, Kenya

XS
SM
MD
LG