Polisi huko Hamburg, Ujerumani, wanasema wanaendelea kutafuta kilichopelekea shambulizi la bunduki la Alhamisi katika Kanisa la Jehovah Witnesses.
Mtu mmoja aliyekuwa na bunduki alifyatua risasi kwenye kanisa, na kuua watu kadhaa, na kujeruhi wengine.
“Hadi sasa hakuna taarifa za kuaminika juu ya kilchopelekea uhalifu huo,” polisi walisema.
Polisi hawajatoa idadi rasmi ya waliouawa, lakini ripoti za vyombo vya habari nchini Ujerumani zinasema watu saba waliuawa katika shambulizi hilo na watu wanane wamejeruhiwa.
Polisi wanasema wanaamini mtu huyo aliyekuwa na bunduki ni kati ya waliofariki na kuwa alifanya shambulizi hilo peke yake.
Chansela Olaf Scholz alilaani “kitendo hicho cha kikatili” na alisema mawazo yake yako pamoja na waathirika na familia zao.
Ujerumani imekuwa ikilengwa na mashambulizi katika miaka ya karibuni na wanajihadi na vikundi vya mrengo wa kulia.
Baadhi ya taarifa katika habari hii inatokana na mashirika ya habari ya AFP na Reuters.