Paul Mackenzie, kiongozi wa kanisa la Good News International, yuko chini ya ulinzi akituhumiwa kwa kosa la kuwaamuru wafuasi wake kuwaweka na njaa watoto wao ili waende mbinguni kabla ya mwisho wa dunia, ambayo aliitabiri kuwa ni tarehe 15 Aprili.
Huku mamia ya watu bado wakidhaniwa kupotea, operesheni ya msako katika msitu wa Shakahola uliopo kusini mashariki mwa Kenya imeanza tena baada ya kusimamishwa kwa siku chache kwa sababu ya hali mbaya ya hewa, alisema waziri Kindiki wakati wa ziara yake.
Wakati huo huo Shirika la habari la AFP linaripoti kuwa uchunguzi wa maiti zilizopatikana kwenye makaburi ya halaiki yanayohusishwa na dhehebu la kidini nchini humo unaonyesha kuwa baadhi ya miili haina viungo, hivyo kuibua tuhuma za uvunaji wa lazima wa viungo, wachunguzi walisema, wakati duru mpya ya ufukuaji ikitarajiwa kuanza siku ya Jumanne.
Polisi wanaamini kuwa miili mingi ni ya wafuasi wa anayejiita kasisi Paul Nthenge Mackenzie anayedaiwa kuwaamuru wafuasi wake wafe kwa njaa "ili wakutane na Yesu."
Nyaraka zilizowasilishwa mahakamani siku ya Jumatatu zilisema kuwa baadhi ya maiti zilitolewa viungo vyao, huku polisi wakidai kuwa washukiwa hao walikuwa wakijihusisha na uvunaji wa lazima wa viungo vya mwili.
"Ripoti za uchunguzi wa maiti hizo zimethibitisha viungo kukosekana katika baadhi ya miili ya waathirika waliokuwa wamefukuliwa," inspekta mkuu Martin Munene alisema katika hati ya kiapo iliyowasilishwa katika mahakama ya Nairobi.
Waendesha mashtaka wanaomba kumshikilia kwa siku nyingine 90 baba huyo wa watoto saba ambaye ni mwanzilishi wa Kanisa la Good News International mwaka 2003 hadi uchunguzi utakapokamilika.
Hakimu mkuu mwandamizi Yusuf Shikanda alisema atatoa uamuzi kuhusu ombi hilo siku ya Jumatano.
Chanzo cha habari hii ni Shirika la habari la Reuters na AFP.