Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 20:02

Marekani yawawekea vikwazo maafisa wa Uganda


Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken

Serikali ya Marekani imetangaza masharti ya visa kwa baadhi ya maafisa wa Uganda ambao wanaaminika walihusika au walishiriki katika kudumaza utaratibu wa kidemokrasia katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

Maafisa hao walihusika na vitendo hivyo wakati wa uchaguzi mkuu wa Januari 14, 2021, na katika kipindi chote cha kampeni kuelekea upigaji kura.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken amesema vitendo vya serikali ya Uganda vimebainisha kuendelea kushuka kwa demokrasia na heshima kwa haki za binadamu vitu ambavyo vinalindwa na Katiba ya Uganda.

Amesema wagombea wa upinzani mara kwa mara walinyanyaswa, kukamatwa na kushikiliwa kinyume cha sheria bila ya kufunguliwa mashtaka. Vile vile majeshi ya usalama nayo yalihusika na vifo na kujeruhi dazeni ya raia wasiokuwa na hatia na wafuasi wa upinzani pamoja na wana habari, kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Wanajeshi wakiwa eneo la mgombea urais wa upinzani Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine, huko Magere, Uganda, on Januari 15, 2021
Wanajeshi wakiwa eneo la mgombea urais wa upinzani Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine, huko Magere, Uganda, on Januari 15, 2021

Jumuiya za kiraia na wanaharakati wanaounga mkono taasisi za uchaguzi na mchakato wa wazi wa uchaguzi wamekuwa wakilengwa kwa kubughudhiwa, kutishwa, kukamatwa, kuondolewa nchini, na mshataka holela na kufungiwa akaunti za benki.

Hatua ya serikali kuzuia waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa na wa ndani ya nchi na jumuiya za kiraia, na wale walioweza kufuatilia mchakato wa uchaguzi walieleza kuwepo kwa dosari kote nchini kabla, wakati na baada ya uchaguzi, ambao umepelekea kutokuwepo uhalali wa uchaguzi huo.

Tume ya uchaguzi ya Uganda ikiongozwa na Simon Byabakama wamaliza kutangaza matokeo ya uchaguzi
Tume ya uchaguzi ya Uganda ikiongozwa na Simon Byabakama wamaliza kutangaza matokeo ya uchaguzi

Mchakato huu wa uchaguzi haukuwa huru wala wa haki. Hata hivyo tunaendelea kuzisihi pande zote husika kutoshiriki katika ghasia na kuheshimu uhuru wa kujieleza, kukusanyika na kusafiri.

Serikali ya Uganda ni lazima iboreshe ipasavyo rekodi yake na iwachukulie hatua wale wote waliohusika kusababisha dosari za uchaguzi, uvunjifu wa amani na vitisho.

Taarifa ya Blinken imesema Marekani itaendelea kutathmini hatua za ziada dhidi ya wahusika waliodumaza demokrasia na haki za binadamu nchini humo, pamoja na familia zao za karibu. Imeitaka serikali ya Uganda kuboresha rekodi yake na kuwawajibisha wote waliohusika na vitendo hivyo.

Taarifa hiyo pia imesema Serikali ya Marekani inahimiza kuwa : “tuwaunge mkono kwa nguvu zote wananchi wa Uganda, na tuendelee na ahadi ya kushirikiana kuendeleza demokrasia na mafanikio ya pamoja kwa nchi zetu,”

XS
SM
MD
LG