Bobi Wine ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi mwenye umri wa miaka 38 ameyapinga matokeo hayo na kusema anaamini kwamba ushindi wake uliibiwa.
Wakili wa chama cha Bobi Wine cha National Unity Platform -NUP, George Musisi amesema Wine anaitaka mahakama kubadili matokeo hayo katika misingi inayohusu kusambaa kwa matumizi ya ghasia.
Museveni ambaye ameliongoza taifa hilo la Afrika Mashariki tangu mwaka 1986, alitangazwa mshindi wa uchaguzi wa Januari 14 kwa kupata asilimia 59 ya kura wakati Wine alipata asilimia 35.
Musisi amesema wanataka matokeo yafutwe na upigaji kura urejewe.
Wakili huyo amesema kuwa kulikuwa na wizi wa dhahiri wa kura kwa maboksi kujazwa kura, kunyanyaswa kwa mawakala wa NUP na wafuasi wake, baadhi yao kukamatwa katika mkesha wa siku ya uchaguzi.
Wine ambaye hilo ni jina lake la kisanii aliwavutia vijana wengi nchini na kusambaza muziki wake kwa waganda na hivyo kujipatia kundi kubwa la vijana waliomuunga mkono na kuwa changamoto kubwa kwa Museveni.