Akizungumza kupitia ukurasa wake wa Youtube kutoka nyumbani kwake anakozuiliwa na wanajeshi wa Uganda UPDF, Bobi Wine alitaka wafuasi wake kujitokeza kwa wingi kote nchini na kuandamana kwa amani, bila kuvunja sheria yoyote, akisema kwamba kwa kufanya hivyo, watakuwa wanadai haki yao ya kikatiba.
Amesema kwamba hatakubali kunyamazishwa na polisi ambao wamemtaka kusema wazi kwamba hataitisha maandamano.
“Nimesikia polisi wakiniambia kwamba niwaambie watu wangu wasifanye maandamano ndipo waniachilie huru. Hilo sio jukumu langu. Raia wa Uganda wanajua kwamba hawajavunja sheria yoyote.”
Bobi wine amesisitiza kwamba alishinda uchaguzi mkuu uliofanyika Januari 14 mwaka huu 2021.
Tume ya uchaguzi ilimtangaza rais Museveni kuwa mshindi wa uchaguzi huo kwa asilimia 58.64 ya kura zilizopigwa. Bobi Wine alipata asilimia 34.83.
Bobi Wine, amedai kwamba chama chake cha National Unity Platform, kina ushahidi wa kutosha kwamba udanganyifu mkubwa wa kura ulifanyika na kumpa ushindi rais Museveni.
“Huu uchaguzi ulikuwa na udanganyifu mkubwa kuliko uchaguzi wa mwaka 1980 ambao Museveni alidai ulikuwa na wizi wa kura na kumfanya kuanzisha vita vilivyodumu miaka 5 na kuingia madarakani kupitia mapinduzi. Haya ni madharau makubwa kwa watu waliopoteza maisha wakati Museveni alikuwa anaongoza vita kwa kile alikuwa amedai kwamba aliibiwa kura. Haya ni madharau makubwa kwa demokrasia.” Amesema Bobi Wine.
Amesema kwamba anaendelea kushauriana na wanasiasa wengine iwapo anastahili kuwasilisha kesi mahakamani kupinga matokeo hayo.
“Tumekuwa tukipata ushauri mbalimbali iwapo tunastahili kwenda mahakamani kupinga matokeo hayo. Tunajua kwamba majaji wote wameteuliwa na Museveni na kuwasilisha kesi mahakamani vile vile ni sawa tu na kuhalalisha ushindi wa Museveni kisheria. Bado tunafikira cha kufanya.” Ameeleza Bobi Wine akiongezea kwamba “Polisi wamechukua baadhi ya ushahidi tuliokuwa tumekusanya walipovamia ofisi zetu na wamekubali kuchukua Ushahidi huo lakini wamekatakaa kurejesha vitu walivyochukua katika ofisi yetu.”
Bobi wine, ametaja majina ya wafuasi wake kadhaa wanaozuiliwa na maafisa wa usalama na hadi sasa hawajulikani walipo. Amedai kwamba polisi na wanajeshi wanaendelea kukamata wafuasi wake na maafisa wa chama chake bila kutoa maelezo yoyote.
Wanaokamatwa wanachukuliwa kutoka nyumbani kwao, alisema Bobi Wine.
Rais Museveni alihutubia taifa baada ya kutangazwa mshindi, na kudai kwamba uchaguzi huo haukuwa na udanganyifu wowote, na ndio wa kwanza wa huru na haki kuwahi kufanyika Uganda.
Huduma ya internet ilizimwa wakati wa uchaguzi na matokeo yalipokuwa yakitolewa lakini kurudishwa baadaye.
Tangu huduma ya intenet iliporudishwa, video vimekuwa zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha ‘polisi na wanajeshi wakihusiaka katika wizi wa kura.’
Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC.