Lt Jenerali Alex Grynkewich, kamanda wa kikosi cha 9 cha jeshi la anga la Marekani huko Mashariki ya Kati, alisema ndege za kivita za Russia zilidondosha miamvuli mbele ya drone za Marekani, ambazo zilizilazimisha droni hizo kuchukua mwelekeo mwingine.
Grynkewich pia alisema moja ya marubani wa Russia alijipenyeza mbele ya droni hiyo na kuziwasha machine kuongeza nguvu ya mwendo wake, ambapo iliathiri uwezo wa droni kufanya kazi yake kwa usalama.
“Tunayasihi majeshi ya Russia nchini Syria kuacha vitendo vya kizembe na kufuata viwango vinavyotegemewa kwa jeshi la anga lenye weledi ili tuweze kurejesha lengo letu la pamoja la kuwashinda ISIS,” Grynkewich alisema katika taarifa yake.
Jeshi la Marekani halikubainisha wapi nchini Syria tukio hilo lilitokea.
Kuna takriban wanajeshi 900 wa Marekani waliopelekwa Syria kwa ajili ya kushauri na kuyasaidia majeshi yanayoongozwa na Wakurdi wanaopigana kulishinda kundi la Islamic State.
Baadhi ya taarifa katika ripoti hii zinatokana na mashirika ya habari ya AP na AFP.
Forum