Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Julai 09, 2024 Local time: 02:10

Marekani yapongeza mpango wa kusitisha mapigano DRC


Wapiganaji nchini DRC.
Wapiganaji nchini DRC.

Marekani imepongeza usitishwaji wa muda wa wiki mbili kwa mapigano mashariki mwa DRC, kwa sababu za kibinadamu, White House imesema. Mapigano makali yamekuwa yakiendelea kati ya wanajeshi wa serikali na waasi wa kundi la M23, wanaoungwa mkono na Rwanda.

Mapigano hayo katika jimbo la Kivu Kaskazini yamepelekea takriban watu milioni 1.7 kutoroka makwao, na kufanya idadi ya watu waliofurushwa makwao nchini humo kufikia milioni 7.2, kwa mujibu wa makadirio ya Umoja wa Mataifa.

Usitishwaji huo wa mapigano, unaoanza saa sita usiku saa za huko, na kwendelea hadi tarehe 19 mwezi huu, utatekelezwa hususan katika maeneo ambayo vita hivyo vinaathiri raia, kwa mujibu wa White House.

Serikali za DRC na Rwanda zimeelezea uungaji mkono wa hatua hiyo, ya kupunguza maumivu kwa raia na kuweka msingi wa kutafuta suluhu la mzozo huo, msemaji wa baraza la usalama wa kitaifa la Marekani Adrienne Watson alisema katika taarifa.

Umoja wa Mataifa na mataifa ya magharibi yamekuwa yakiishutumu Rwanda kwa kuunga mkono kundi la M23, lakini Rwanda imekuwa ikikanusha tuhuma hizo.

Alhamisi, askari 25 walihukumiwa kifo na jopo la kijeshi la DRC, baada ya kupatikana na hatia ya kutoroka vita, na wizi, kwa mujibu wa mawakili wao.

Forum

XS
SM
MD
LG