Wanawake pia wameitaka serikali ya mapinduzi ya Zanzibar kuunda taasisi maalumu itakayo weza kusimamia shughuli za wanawake ili waweze kujikomboa kiuchumi.
Juhudi za wanawake zimeendelea kuonekana katika kipindi ambacho wanawake wengi wanakabiliwa na changamoto mbalimbali wakati huo huo wakiitaka jamii kuangalia mila na desturi ambazo zimekuwa si rafiki kwao na kuwafanya kuendelea kuwa tegemezi hali ambayo inawarudisha nyuma na kuendelea kudharaulika katika jamii inayo wazunguka
Licha ya juhudi kubwa wanazofanya kujikomboa kiuchumi lakini bado ndani ya jamii pamekuwa na mitazamo hasi hasa inapo fika kipindi cha kuolewa imekuwa ni miongoni mwa sababu kwa wanaume wengi kuwarudisha nyuma kwa kutumia mamlaka waliopewa kama sehemu ya kukwamisha ndoto za wanawake walio ndani ya ndoa kama anavyo sema Saumu Mohamedi mkazi wa Magogoni wilaya ya Magharibi B .
‘‘wanawake wengi wametayarishwa na wazazi wao wasiwe wafanyakazi wala wafanya biashara lakini kutokana na uchumi ulivyo kuwa mgumu baadhi ya wanawake wanajitolea kufanya kazi pamoja na kuwa wanajitokeza kujikomboa kiuchumi lakini wanakumbana na changamoto nyingi kwa mfano mwanamke kuolewa ni baraka na bahati lakini ni kikwazo kwa sababu mwanaume ndio kesha ambiwa kwamba yeye ndio atakuwa msimamizi wa yule mwanamke’’ ameongezea kusema Saumu Mohamedi
Wanaume wataendelea kutajwa hadi pale watakapo amua kumuacha mwanamke huru na kufanya kile anacho hitaji katika jamii yake hali ambayo inaonekana kwa Zanzibar itachukua muda mrefu zaidi kwa vile wanaume wengi wanaamini kuwa kazi ya mwanamke ni kuihudumia familia na kuhakikisha malezi ya watoto yanabaki salama kupitiakatika mikono yake
Hali hiyo inawafanya wanawake kuendelea kuwa wategemezi hata pale wanapo amua kuanzisha miradi wanakosa usimamizi jambo linalo sababishwa na wanaume zao kuwakataza kufanya shughuli yoyote ilio nje ya nyumbani Aysha Makame mwenyeji wa Unguja ameiambia Sauti ya Amerika ili wanawake wajikwamue basi serikali ya mapinduzi ya Zanzibar inapaswa kuunda taasisi itakayo weza kusimamia na kuratibu shughuli zao zote.
‘‘kungekuwa na wasimamizi maalumu wakuwasimamia wakina mama wenye vikundi vyao vya ushirika mfano kama hawa wakulima wa mwani wawe na wakuu wao serikalini wanawasimamia ili kuona wao kila mwezi wanaingiza kiasi gani basi kina mama leo hii wangekuwa wako juu zaidi ya wafanyakazi walio ajiriwa’’aliongezea Aysha
Hata hivyo mkurugenzi kutoka bodi ya huduma za maktaba katika wizara ya elimu na mafunzo ya amali Zanzibar Ulfati Abdulaziz amesema wanawake wapo katika nafasi mbalimbali za uongozi na wengine wakijihusisha na masuala ya biashara japo pana baadhi ya familia zinapaswa kubadili mitazamo na tabia ya kumfanya mwanamke kuwa mama wa nyumbani na badala yake watumie mfano wa Rais wa Tanzania ambaye ni kiongozi wa nchi.
“mwanamke nikiumbe ambae anatakiwa akae tu ndani apike au amshuhulikie mme hivyo ni vitu vya zamani ni vitu ambavyo vimepitwa na wakati ukiangalia Rais wetu wa Tanzania ni mwanamke na sio tu mwanamke ni Mzanzibar kama ndio kungekuwa na utamaduni huo sidhani kama leo tungekuwa na Rais mwanamke kutoka Zanzibar” alisema Ulfati
Siku ya wanawake imeadhimishwa Zanzibar kwa wanawake kusherehekea mafanikio na kutatua changamoto zinazo wakabili na kutakiwa kutumia majukwaa ya kidigitali kupaza sauti zao kwa kuongeza maarifa na ujuzi ameongezea kusema Ulfati Abdulaziz
Imetayarishwa na mwandishi wetu Amri Ramadhani, Dar es Salaam, Tanzania.