Kimbunga hicho kilisababisha mafuriko, na vyombo vya habari viliripoti kwamba miti na magari yalionekana yakisombwa na maji huku nyumba kadhaa katika maene mbalimbali zikiharibiwa.
Ian kilitua Jumatano kusini-magharibi mwa Florida, na kimetajwa na wataalam kama mojawapo ya dhoruba zenye nguvu zaidi kuwahi kurekodiwa nchini Marekani.
Kituo cha vimbunga cha Marekani kilisema dhoruba hiyo, ya kiwango cha nne, ilitua karibu na Cayo Costa, kisiwa kilichohifadhiwa magharibi mwa Fort Myers, mji wenye wakazi wengi, ikiwa na kasi ya kilomita 241 kwa saa.
Kimbunga hicho kimesababisha mafuriko katika eneo kubwa la Florida huku kikielekea kaskazini mashariki mwa pensula ya kaskazini Magharibi.
Serikali ya jimbo hilo na ile ya Marekani, awali zilitoa tahadhari kwa wakazi wa maeneo yaliyolengwa na dhoruba hiyo, huku wakazi wengi wakilazimishwa kuondoka kutoka kwa makazi yao, ili kuhakikisha uslama wao.
Maafisa wamesema angalau watu milioni moja na nusu wamebaki bila umeme kutokana na kimbunga hicho.