Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Desemba 27, 2024 Local time: 07:39

Kenyatta amuidhinisha rasmi Raila Odinga kugombea urais Kenya


Kiongozi wa chama cha Upinzani cha ODM, Raila Odinga (Kushoto) na Rais Uhuru Kenyatta.
Kiongozi wa chama cha Upinzani cha ODM, Raila Odinga (Kushoto) na Rais Uhuru Kenyatta.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta Jumamosi alimuidhinisha rasmi mpinzani wake wa zamani wa kisiasa kushika wadhifa wa juu zaidi wa nchi hiyo, Raila Odinga, wiki kadhaa baada ya vyama vyao kuungana pamoja kabla ya uchaguzi wa rais na bunge wa mwezi Agosti mwaka huu.

Kwenye hafla iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa KICC mjini Nairobi, takriban vyama kumi na sita vya kisiasa, vilimuidhinisha Odinga kupeperusha bendera ya muungano huo.

"Tumemchagua Raila Odinga bila upinzani wowote kuwa rais wa tano wa Kenya," Kenyatta aliuambia umati wa maelfu uliokuwa ukishangilia kwa shangwe na vigelegele.

Ingawa Kenyatta alikuwa ameelezea azma yake ya kumuunga mkonoi Odinga katika hafla za awali, tangazo hilo rasmi sasa linawaleta pamoja viongozi wawili wakuu wa kisiasa nchini Kenya, ambao wana historia ndefu ya kupambana kisiasa.

Mnamo mwaka wa 2018, Kenyatta na Odinga waliishangaza nchi walipopeana mikono, katika kile kilichokuja kujulikana kama 'Handshake' na kutangaza kusitisha mapigano baada ya ghasia za baada ya uchaguzi wa 2017, kusababisha vifo vya watu kadhaa.

Mwezi uliopita, chama cha Kenyatta cha Jubilee kilitangaza kuwa kitajiunga na muungano wa Azimio la Umoja unaoongozwa na Odinga.

Siku ya Jumamosi, Kenyatta alisema: "Hatuna shaka yoyote kwamba tuna nahodha wa timu hii, naye ni Raila Amolo Odinga."

Odinga, mwenye umri wa miaka 77, alijibu, akisema amekubali uteuzi huo na alikuwa na shukran nyingi kwa Wakenya.

Tangazo hilo lilijiri baada ya naibu wa Rais wa nchi hiyo William Ruto, ambaye pia ana nia ya kugombea kiti cha urais, kutimuliwa kutoka kwa chama cha Jubilee.

Ruto, aliyehamia chama cah United Democratic Alliance, UDA, anatajwa na wachambuzi kama mpinzani mkuu wa Odinga, kwelekea kwa uchaguzi wa mwezi Agosti.

"Hizi ni mbio za farasi wawili ambao ni Raila Odinga wa ODM na William Ruto wa UDA. Wengine wanapoteza wakati wao," alisema Profesa Herman Manyora, mchambuzi wa siasa za Kenya.

Kwa kuwa wengi wa Wakenya hupiga kura kwa misingi ya kikabila, chaguzi nchini Kenya mara nyingi zimekumbwa na ghasia, kwa mujibu wa shirika la habari la AFP.

Zaidi ya watu 1200 walipoteza maisha yao kufuatia uchaguzi wa mwaka wa 2007, ambao uligubikwa na ghasia na umwagikaji wa damu kwa kiwango ambacho hakikuwa kimeshuhudiwa katika historia ya taifa hilo la Afrika Mashariki.

XS
SM
MD
LG