Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Desemba 27, 2024 Local time: 07:49

Ruto adai njama za kukataa kumtambua kama rais iwapo atashinda uchaguzi


Naibu wa Rais wa Kenya William Samoei Arap Ruto.
Naibu wa Rais wa Kenya William Samoei Arap Ruto.

Naibu wa Rais wa Kenya, William Ruto, ambaye pia ni mgombea urais nchini humo, amesema kuna tetesi za mipango ya kukataa kumtangaza kama mshindi wa uchaguzi wa urais, baada ya zoezi kufanyika tarehe tisa mwezi Agosti mwaka huu.

Hali kadhalika mwanasiasa huyo alisema kuna njama za kuizuia jumuiya ya kimataifa, kutoa msaada wa vifaa, na wa kimikakati, kwa tume ya uchaguzi ya na mipaka ya Kenya, IEBC, kujiandaa kwelekea kwa uchaguzi huo mkuu.

Ruto alisema hayo katika mahojiano maalum katika studio za Sauti ya Amerika mjini Washington DC, alipokuwa katika ziara nchini Marekani mwishoni mwa wiki.

"Ni kweli...sio uvumikwamba kuna mipango hiyo. Wengine wamesema waziwazi kwamba Ruto hatafika wakati wa uchaguzi," alisema.

Kuhusu wakimbizi walio nchini Kenya, Ruto alisema iwapo atachaguliwa rais, utawala wake utahakikisha kwamba mchakato wa kuwahamisha wakimbizi kutoka kambi za Kakuma na Daadab utafanyika kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya Kenya, Somalia na UNHCR, na zoezi hilo litakuwa la hiari kwa wale wanaotaka kurudi makwao.

"Ni lazima tutekeleza jukumu latu kama sehemu ya jumuiya ya kimataifa," alsisema.

Alipoulizwa kuhusu shutuma dhidi ya serikali inayoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta, kwamba imekuwa na hulka ya kutotii maamuzi ya mahakama, Ruto alisema atahakikisha kwamba sheria zote zinaheshimiwa.

Aliongeza kwamba iwapo atakuwa rais, atamrejesha nyumbani wakili aliye uhamishoni nchini Canada, Miguna Miguna.

"Huyo Miguna Miguna tuatamrejesha mara moja. Sioni sababu ya kuwa na wakimbizi nchini kwetu wakati mmoja wetu ni mkimbizi nchini Canada," alisema.

Ruto, ambaye aliandamana na mwanasiasa mwingine aliye kwenye muungano wao wa kisiasa wa Kenya Kwanza, Musalia Mudavadi, pia alisema atatumia tajiriba yake kama naibu wa Rais, kuharakisha mchakato wa kuboresha ushirikiano wa Afrika Mashariki.

"Ninaamini kwamba Jumuiya ya Afrika Mashariki ndiyo itasukuma mpango wa soko huria la Afrika, ambalo naliona kama litakalosaidia pakubwa kuwapa ajira watu wetu, likilenga watu bilioni moja barani Afrika," alisema.

Wakati huo huo, mchambuzi wa masuala ya siasa za Kenya Prof Herman Manyola, Jumatatu alisema kwamba mengi ya aliyoyasema Ruto, yalitarajiwa.

"Hizo ni kauli za kisiasa tu. Hauwezi kuamini kila kitu mwanasiasa anakwambia," Manyora alikiambia kipindi cha "Kwa Undani" cha VOA Swahili katika mahojiano.

"Kila mwanasiasa anapopata nafasi atasema kile ambacho anaona kitawafurahisha watu," aliongeza.

XS
SM
MD
LG