Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Desemba 27, 2024 Local time: 12:29

KANU yamuidhinisha Gideon Moi kugombea nafasi ya urais 2022


Senetor Gideon Moi
Senetor Gideon Moi

Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama cha KANU nchini Kenya, wamemuidhinisha Gideon Moi, kugombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2022.

Moi ameeleza kuwa iwapo atapata ridhaa ya raia wa Kenya kwenye uchaguzi ujao, ataongoza serikali inayowajumuisha wote na vile vile kupambana na ufisadi.

Kongamano hilo la Kitaifa la wajumbe limemuidhinisha Seneta huyo wa jimbo la Baringo kuwa mgombea urais kumrithi Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi wa mkuu wa mwaka 2022.

Moi mwenye umri wa miaka 57, ni mwanasiasa na mwanawe hayati Daniel Arap Moi aliyekuwa rais wa pili wa Kenya kwa miaka 24 kati ya mwaka 1978 na 2002.

Daniel Arap Moi wa Kenya
Daniel Arap Moi wa Kenya

Moi pia ni mwenyekiti wa chama cha KANU, ambacho ndicho chama kilichotwaa madaraka kutoka mikononi mwa wakoloni na kuwa chama cha kwanza baada ya Kenya kupata uhuru.

Tangu mwaka 2013, Moi amekuwa akiwakilisha jimbo la Baringo lililopo Magharibi ya Kati ya Kenya na sasa ameonyesha nia ya kugombea urais, kuitawala Kenya kama alivyofanya babake chini ya chama hicho.

Mwaka 2013 na tena mwaka 2017, chama cha KANU kilimpigia debe Rais aliyepo madarakani Uhuru Kenyatta, kuiongoza Kenya kwa mihula miwili madarakani.

Gideon Moi anajitosa kwenye kinyang’anyiro cha urais, jukwaa ambalo linashuhudia viongozi mbalimbali wa kisiasa waliokuwa ndani ya chama hicho miaka ya nyuma kama vile Naibu Rais wa Kenya William Ruto, Raila Odinga, Kalonzo Musyoka na Musalia Mudavadi, wote ambao wameonyesha nia ya kuwania kwa tiketi ya vyama tofauti kumrithi Rais Kenyatta, anayetarajiwa kustaafu mwaka 2022 baada ya kuwa madarakani kwa kipindi cha miaka kumi.

Mark Bichache, Mfuatiliaji wa siasa za Kenya anaeleza kuwa japo Moi hana nguvu tosha za kisiasa, hafai kupuuzwa.

Kiongozi wa cha Orange Democratic Movement Raila Odinga, aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, akizungumza katika hafla hiyo, ameeleza kuwa anaunga mkono kuwapo kwa uhuru wa vyama vya siasa kudumisha demokrasia ya vyama vingi na kwamba anajivunia mwamko wa siasa za Kenya.

Kalonzo Musyoka aliyekuwa Katibu Mtendaji wa chama hicho, na sasa kiongozi wa Wiper Democratic, ameeleza kuwa historia ya KANU ni chimbuko bora la historia ya Kenya.

Kiongozi wa Amani National Congress Musalia Mudavadi, ameeleza kuwa vuguvugu la kisiasa liitwalo One Kenya Alliance ambalo pia linamjumuisha Bw Moi, limepata nguvu mpya kuelekea uchaguzi mkuu.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Kennedy Wandera, Nairobi, Kenya

XS
SM
MD
LG