Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Desemba 28, 2024 Local time: 05:22

Kenya: Naibu Rais Ruto asema serikali inamdhalilisha na kumdunisha


Naibu wa Rais wa Kenya William Ruto (Kulia)
Naibu wa Rais wa Kenya William Ruto (Kulia)

Naibu Rais wa Kenya William Ruto, Jumatano alieleza kuwa hatua ya serikali kumzuia kufanya safari ya kibinafsi nchini Uganda Jumatatu wiki hii ni njama ya kimakusudi ya kumdunisha na kumdhalilisha mbele ya macho ya umma.

Kiongozi huyo ambaye uhusiano wake na rais wa taifa hilo Uhuru Kenyatta umeonekana kudorora zaidi, ameeleza kuwa kwa kipindi cha miaka tisa amekuwa serikalini katika wadhifa wake wa naibu rais, hajawahi kuhitaji idhini ya kusafiri nje ya mipaka ya Kenya na kinachotukia ni siasa za uchaguzi wa mwaka 2022.

Wakati kuzuiliwa kwake kuelekea Uganda kukiendelea kuibua hisia za kisiasa nchini Kenya, Ruto mwenyewe ameeleza kuwa kuzuiliwa huko kuna nia ya kumhujumu na kuvuruga uwezo wake serikalini na watu walio karibu na Rais Kenyatta.

"Yale yaliyofanyika pale kwenye uwanja wa ndege, ni kujaribu kunidunisha. Kuonyesha kwamba sina maana," alisema.

Katika mahojiano ya kipekee yaliopeperushwa na Televisheni ya Citizen jijini Nairobi Jumatano asubuhi, Ruto alinung’unikia kile anachokitaja kuwa ni kuendelea kuwapo kwa matatizo chungu nzima katika serikali walioweka pamoja na rais Kenyatta lakini licha ya kuwa kwenye serikali hiyo, Ruto anakiri Kenyatta hajamkinga dhidi ya matatizo haya.

Ruto ambaye ametangaza kugombea urais kumrithi Kenyatta katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022, anasema hajawahi kutafuta idhini ya Kenyatta kufanya safari nje ya mipaka ya Kenya. Na kwamba iweje, sasa hivi aelezwe hahitaji kuondoka bila kutimiza itifaki zote serikalini?

"Nimetembea nchi nyingi kwa ziara rasmi na ziara binafsi na sijawahi kuambiwa nahitaji kibali cha kusafiri," alieleza.

Ruto anaeleza kuwa kilichotukia Jumatatu mchana ni muendelezo wa msururu wa masaibu ambayo anayapitia katika serikali ya Kenyatta, huku akikiri kuwa Kenyatta alimkabidhi waziri wa usalama wa ndani Fred Matiang’I majukumu yake ya kikatiba.

Kwenye ujumbe wa Bw Ruto, vyombo vya habari vya Kenya vinaripoti alikuwepo mfanyabiashara raia wa Uturuki Harun Aydin, mwenye umri wa miaka 54 ambaye vyombo vya habari vya Kenya vinaripoti amesafiri mara kadhaa na Bw Ruto. Kwa mujibu wa gazeti la Nation Africa nchini Kenya, Harun Aydin amekuwa akisafiri mara kadhaa na Ruto kuenda Zanzibar, Uganda na Sudan lakini licha ya kufanya safari nyingine kutoka Istanbul, Cairo na Addis Ababa kuingia Nairobi, mienendo yake haifahamiki. Lakini Ruto anaeleza huyu ni mfanyabiashara na mwekezaji mashuhuri.

Kwa miezi ya hivi nyuma, uhusiano wa Ruto na rais wa Uganda Yoweri Museveni umeonekana kunawiri. Tangu Kenyatta na Ruto kushika hatamu za uongozi 2013, Ruto amesafiri Uganda mara kadhaa, ziara ya mwisho imejiri Julai mwaka huu alipokutana na Museveni kuzindua kiwanda cha kutengeneza chanjo wilaya ya Wakiso, hii ikiwa ni ziara ya tano katika kipindi cha miaka sita. Bw Ruto anasema wanaomkosoa kwa mahusiano yake na Museveni wanakosea.

Lakini Je, matamshi haya ya Ruto yanauweka wapi ushawishi na nafasi yake katika serikali ya Rais Kenyatta? Swali hili nimemuuliza Professa Hezron Mogambi, mhadhiri katika chuo kikuu cha Nairobi na mfuatiliaji wa siasa za Kenya.

"Inaashiria hadhi yake kushuka katika serikali amabayo waliiunda na Rais Kenyatta mwaka wa 2013 na ushawishi wake umeendelea kushuka," alisema Prof Mogambi.

-Imetayarishwa na Kennedy Wandera, VOA, Nairobi, Kenya

XS
SM
MD
LG