Kampuni hiyo ya Kandia Fresh, imezuiliwa kufanya biashara zake Njombe, kusini mashariki mwa Tanzania, baada ya kudaiwa kununua matunda kabla hayajakomaa.
Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, amesema kampuni hiyo ilipigwa marufuku mara baada ya kudaiwa kununua maparachichi kabla ya kuiva na kuyatupa katika jalala lililopo katika halmashauri ya mji wa Njombe.
“Kama kampuni hiyo ipo nchini, iondolewe haraka, ifutiwe kibali chao” alisema Bashe.
Baadaye aliamuru kukamatwa kwa mfanyakazi wa kampuni hiyo David Sifuna Barasa,ambaye alishiriki katika manunuzi ya maparachichi kupitia madalali na bila kibali.
Parachichi ghafla limekuwa zao jipya adimu la Tanzania. Kwa mujibu wa Umoja wa kilimo cha Bustani , katika kipindi cha 2021 Tanzania ilisafirisha zaidi ya tani 11,237 za maparachichi yenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 33.
Mwaka huu Tanzania inatarajiwa kusafirisha tani 15,000 na kuzalisha fedha za kigeni dola za Kimarekani millioni 45. Takwimu zinaonyesha Ulaya inaingiza asilimia 85 ya maparachichi kutoka Tanzania. Ufaransa inaongoza kwa kuiingiza maparachichi mengi ikifuatiwa na uholanzi, halafu Uingereza.
Chanzo cha habari hii ni gazeti la "The East African" linalochapishwa Kenya