Wakidai waathirika waliuawa kwa kupigwa risasi baada ya kukutwa katika maeneo ya mgodi huo huku wakishangazwa na ukimya wa serikali katika kukemea vitendo hivyo.
Wakati hali ya wasiwasi ikizidi kuongezeka miongoni mwa wananchi wanaoishi katika maeneo hayo, mmoja wa wakazi wa eneo hilo Anna Julius mjane anayeishi katika kijiji cha Nyamongo na ni mama wa watoto watatu ameiambia Sauti ya Amerika kuwa kwa sasa amelazimika kuishi na wakwe zake baada ya mume wake kuuawa kwa kupigwa risasi na askari wanaoulinda mgodi huo wa dhahabu.
Mjane huyo ameeleza mume wake alipigwa risasi tarehe 26 Desemba akiwa katika harakati za kutafuta riziki katika maeneo ya mgodi huo, hali iliyomsababisha kuishi katika mazingira magumu yeye na watoto wake kutokana na kifo cha mume wake.
“Mume wangu baada ya kufariki toka tarehe 26 Desemba kwenye mgodi wa Nyarugusu, shida ambayo nipo nayo sasa hivi ni kubwa sana. Ningeomba tu msaada wenu kwa sababu mume wangu aliuwawa kwenye kutafuta baada ya kupigwa risasi. Mimi naomba ushirikiano wenu,” alisema Julius
Kwa mujibu wa Afisa Madini Mkoa wa Mara,Amini Msuya, mgodi huo wa North Mara unaingizia serikali takribani shilingi bilioni tisa kwa mwezi kutokana na makusanyo ya mirahaba na ada ya ukaguzi, lakini licha ya kuingiza mapato hayo, wananchi wa maeneo hayo bado wamekuwa wakikosa huduma za jamii ikiwa ni pamoja na maji, umeme, na elimu, suala ambalo linawafanya kushindwa kuona faida ya mgodi huo.
Samweli Gikalo ni mkazi wa Nyamongo ambaye pia mdogo wake aliuawa na polisi wa mgodi huo amesema serikali imekuwa ikikaa kimya baada ya kutokea kwa mauaji hayo bila kutoa kauli za kukemea vitendo hivyo hali inayoendelea kuleta wasiwasi.
“Kwa nini watu wanaouawa hovyo hovyo kama wanyama? Ndio maana tunataka serikali ije lakini hakuna mtu wa serikali aliyekuja hata mmoja na mpaka hapo mtu akiwa anaulizia serikali ni kama serikali haipo.”
“Serikali imebaki ni serikali ya kulinda muwekezaji tu, inamaanisha raia na haki za binadamu wao hawajali chochote,” aliongeza.
Ofisa huyo wa madini wa mkoa wa Mara aliiambia Sauti ya Amerika kuwa, matukio hayo yamekuwa yakijitokeza baada ya baadhi ya wananchi kujiwekeaa utaratibu wa kuvamia maeneo ya mgodi huo na kuchukua sehemu ya mabaki ya dhahabu na hivyo kusababisha mapigano kati yao na polisi.
“Wananchi wa mgodi huo wamekuwa na changamoto za uvamizi kwenye maeneo ya mgodi. Wamekuwa wakivamia kwenda kuchukua mawe yanayosadikiwa kuwa na dhahabu, na changamoto hiyo imepelekea kuwa na athari mbalimbali ikiwemo vijana kuumia na vijana wengine kufariki. Hii inatokana na mapigano kati ya wananchi na polisi ambao wanalinda mgodi ule,” alisema afisa huyo wa madini.
Hata hivyo alisema serikali inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kwa kuwaeleza kwamba hawaruhusiwi kufanya uvamizi katika maeneo ya mgodi. Serikali pia inaandaa mpango wa kufufua migodi mingine ili kuwatafutia ajira wananchi hao.
Imetayarishwa na Amri Ramadhani, Sauti ya Amerika, Dar es Salaam.
Forum