Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 14:02

Kampeni za kinyang'anyiro cha Uchaguzi Marekani 2020 zaelekea ukingoni


FILE - Rais Donald Trump, kushoto, na Makamu wa Rais wa zamani Joe Biden
FILE - Rais Donald Trump, kushoto, na Makamu wa Rais wa zamani Joe Biden

Kampeni za uchaguzi mkuu hapa Marekani zimepamba moto ikiwa zimebaki karibu wiki mbili kabla ya watu kwenda kupiga kura hapo Novemba 3, huku Rais Donald Trump na mpinzani wake Joe Biden wakitembelea majimbo yenye ushindani mkali katika siku hizi za mwisho.

Kila mgombea anataka kuhakikisha anapata ushindi katika majimbo hayo muhimu kuweza kushinda kwenye uchaguzi ambao tayari zaidi ya watu milioni 27 wameshapiga kura zao.

Wagombea hao wa kiti cha urais, Donald Trump wa chama cha Republican na Makamu wa Rais wa zamani, Joe Biden, mgombea wa chama cha Demokratik wataendelea na safari zao katika pembe mbali mbali za nchi kueleza sera zao na kuwahimiza wapiga kura kujitokeza kwa wingi zaidi.

Wanasiasa hao wamepangiwa kukutana ana kwa ana siku ya Alhamisi mjini Nashville, jimboni Tennesse kwa mdahalo wa mwisho wa dakika 90.

Masuala muhimu yatakayo jadiliwa kulingana na kamati huru ya midahalo ya rais ni pamoja na masuala ya ubaguzi wa rangi, mabadiliko ya hali ya hewa na vita dhidi ya ugonjwa wa COVID-19.

Na kuhusiana na janga hilo spika wa Baraza la Wawakilishi Nancy Pelosi ameipatia White House hadi Jumanne jioni kuidhinisha mpango wa kunusuru uchumi unaodorora kutokana na janga la virusi vya corona kwa msaada wa kati ya dola bilioni 1.8 hadi bilioni 2.

Spika wa Baraza la Wawakilishi Marekani Nancy Pelosi
Spika wa Baraza la Wawakilishi Marekani Nancy Pelosi

Spika Pelosi akifafanua hilo : "Kwa sababu tunataka kuwepo na makubaliano, kwa hiyo tunaweza kujadiliana na tunaweza kufanya hivi sasa. Kwani kuna tofauti gani kati ya siku mbili au tatu? Inahitaji siku chache tu na tunaweza kukubaliana kabla ya siku ya uchaguzi. Tunaitaka kwa haraka zaidi ikiwezekana."

Mvutano huo ukiendelea zaidi ya watu milioni 27 wameshapiga kura zao katika pembe mbali mbali za Marekani ikiwa ni idadi kubwa katika historia mnamo wakati huu, na zaidi ya mara 6 ya idadi ya watu waliopiga kura kwa njia hii mwaka 2016.

Hadi hivi sasa wilaya zinazodhibitiwa na Wademokrat ndio zimeshuhudia idadi kubwa ya watu waliojitokeza mapema kuliko zile za Warepublikan.

Mbali na kumchagua rais wa Marekani wanapiga kura za kuwachagua wagombea katika bunge la taifa na mabunge ya majimbo pamoja na wajumbe wa serikali za mitaa.

Katika utafiti wa maoni unaonyesha Trump yuko nyuma ya Biden hasa katika majimbo yenye ushindani. Kutokana na hayo baadhi ya Warepublikan wameanza kujitenga na rais au kueleza wasiwasi wao kwamba huenda Biden akashinda. Lakini mwenyekiti wa kamati kuu ya chama cha Republikan Ronna McDaniel anasema Warepulikans watajitokeza siku ya kupiga kura kumchagua rais.

Ronna McDaniel
Ronna McDaniel

Mwenyekiti McDaniel anaeleza : "Tunashuhudia jinsi watu walivyohamasika na tunashuhudia idadi kubwa kabisa ya watu wanaojitokeza kwa ajili ya rais. Haya ni mashindano makali kweli. Na ikiwa kuna Mrepublican yeyote asiyefahamu kwamba kuungana na rais huyu kutamsaidia basi wanajiletea madhara kwa muda mrefu ujao.

Kilicho baki hivi sasa mnamo siku hizi za mwisho kabla siku ya uchaguzi ni kwamba wagombea kiti watajaribu kuwahamasisha wafuasi wao na kutumaini watajitokeza kwa wingi kupiga kura.

XS
SM
MD
LG