Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Agosti 23, 2024 Local time: 11:03

Kagame ashinda katika uchaguzi wa urais Rwanda


Rais wa Rwanda ambaye anagombea tena nafasi hiyo akipiga kura huko Kigali, Julai 15, 2024. Picha na LUIS TATO / AFP.
Rais wa Rwanda ambaye anagombea tena nafasi hiyo akipiga kura huko Kigali, Julai 15, 2024. Picha na LUIS TATO / AFP.

Rais Paul Kagame wa Rwanda ameshinda muhula wa nne katika uchaguzi wa urais na bunge uliofanyika Rwanda Julai 15.

Wapiga kura walikuwa milioni tisa na katika kura milioni saba zilizokwishahesabiwa Rais Paul Kagame amepata asilimia 99.15 ya kura zote.

Frank Habineza wa chama cha Green Party of Rwanda(DGPR) amepata asilimia 0.53 ya kura zilizokwishahesabiwa huku mgombea binafsi wa Phillipe Mpayimana akipata asilimia 0.32 za kura zilizohesabiwa

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi Bi Oda Gasinzigwa amesema kwamba zoezi la kuhesabu kura linaendelea, na Jumanne julai 16 yatatangazwa matokeo ya muda ya uchaguzi wa bunge

Mara baada ya kutangazwa matokeo haya Rais Paul Kagame amewapongeza wananchi wote walioshiriki zoezi la uchaguzi lakini pia akawapongeza kwa namna ya kipekee wakuu wa vyama vya siasa vilivyofanya mseto na chama tawala cha RPF.

‘’Ushindi wa matokeo haya mnaouona ni muungano wa wafuasi wa wanachama wetu wa RPF kwa ushirikiano na wafuasi wa vyama vingine washirika wetu’’ alisema Kagame akiwanyooshea mkono wa shukrani viongozi hao waliokuwa wamesimama nyuma yake.

Kiongozi wa chama cha Green Party of Rwanda Frank Habineza mara baada ya kutolewa matokeo alimpongeza Rais Paul Kagame kwa ushindi huo huku Pillipe Mpayimana mgombea binafsi akisema hata kama hesabu zinaonyesha ameshindwa lakini bado ana imani kwamba atafanya vizuri siku za usoni na kwamba kikubwa kwake ni kwamba alionyesha uzalendo wake kwa kugombea nafasi ya urais.

Zaidi ya watu milioni tisa walijiandikisha katika daftari la wapiga kura huku milioni mbili kati ya hao wakipiga kura kwa mara yao ya kwanza wengi wao wakiwa ni vijana wa chini ya miaka 20

Matokeo haya yanakamilisha mchakato wa kupiga kura na kampeini za uchaguzi ambapo ilitarajiwa kuwa Rais Paul Kagame ambaye ameiongoza Rwanda kwa miaka 24 sasa akitarajiwa kushinda muhula wa nne wa uongozi.

Kagame ambaye ni mwajeshi kitaaluma wakati wa kampeini zake alisema mara kadhaa kwamba angeshinda uchaguzi huo kutokana na mchango wake katika maendeleo ya Rwanda, lakini akibaini kwamba alikubali kugombea ili kukidhi mahitaji ya raia waliomuomba siku zote kugombea tena

Mara baada ya kukamilisha kampeini za uchaguzi alisema kwamba anaendelea kuwaomba wanachama wa chama chake kuendelea kufikiria mtu atakayechukua nafasi yake hapo baadaye kwani kwa maoni yake wakati umefika mtu mwingine achukue hatamu za uongozi.

Rais Kagame anapongezwa kuinua uchumi wa Rwanda na kuihakikishia nchi hiyo usalama wa kutosha lakini mashirika ya haki za binadamu yamekuwa yakiulaumu utawala wake kushindwa kuwavumilia wapinzani. Yeye na serikali yake wanalikanusha hilo wakisema wanaosema hayo ni wale wenye nia mbaya na wanaonuia siku zote kuipaka matope Rwanda

Kwa matokeo haya ni wazi sasa Rais Kagame anaiongoza Rwanda kwa muhula mwingine wa miaka mitano ijayo.

Mwaka 2015 katiba ya Rwanda ilifanyiwa mabadiliko na kumuongezea haki ya kugombea mihula mingine miwili ya miaka mitano, hii ina maana baada ya muhula huu Kagame ana haki kwa mujibu wa katiba ya Rwanda ya kugombea muhula mwingine

Imetayarishwa na Sylivanus Karemera, Sauti ya Amerika, Kigali

Forum

XS
SM
MD
LG