Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Aprili 14, 2025 Local time: 02:23

Ghasia za uchaguzi Msumbiji: Ulinzi waimarishwa katika mji mkuu wa Maputo


Wanajeshi wa Msumbiji wakifanya doria katika mitaa ya mji mkuu wa Maputo huko Msumbiji Novemba 8, 2024. Picha na REUTERS
Wanajeshi wa Msumbiji wakifanya doria katika mitaa ya mji mkuu wa Maputo huko Msumbiji Novemba 8, 2024. Picha na REUTERS

Mji mkuu wa Msumbiji, Maputo ulikuwa mtupu Jumanne, siku ya mkesha wa Krismasi, huku kukiwa na ulinzi mkali katika vituo muhimu vya mji huo, siku moja baada ya mahakama ya katiba kuidhinisha matokeo ya uchaguzi wa Oktoba.

Polisi wakiwa katika magari ya ulinzi wamekuwa wakipiga doria mjini Maputo kufuatia usiku wa ghasia kote nchini baada ya chama tawala cha Frelimo kutangazwa mshindi wa uchaguzi mkuu.

Maduka, mabenki na baadhi ya majengo ya umma yamechomwa moto Jumatatu usiku.

Jumanne rais-mteule Daniel Chapo akishangiliwa na wafuasi wake ameelezea kuridhishwa na matokeo akitoa wito wa maridhiano, alipozungumza kwa mara ya kwanza baada ya matokeo kuhibitishwa ni mshindi wa kiti cha rais kwa kupata asilimia 65 ya kura.

Rais-mteule wa Msumbiji amesema “narudia tena, sisi tutaendelea na majadiliano na watu wote wa Msumbiji kutoka matabaka yote ya kijamii. Viongozi wa miji, viongozi wa kidini, vyama vya vijana, vyama vya wafanyakazi.”

“Waalimu na wafanyakazi wote wa umma na sekta binafsi. Tabaka hizo zote ni muhimu kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu na majadiliano haya yatakuwa msingi wa maendeleo ya nchi yetu” ameongeza.

Kiongozi wa upinzani Venancio Mondlane akizungumza kwa njia ya video iliyobandikwa kwenye ukurasa wake wa Telegram Jumanne, akiwa uhamishoni amesema mahakama ya katiba imehalalisha wizi wa kura, ikihalalisha kudhalilishwa kwa raia wake wenyewe.

“Huu ni wakati muhimu katika maisha yetu, suala ni je tuipange nchi yetu kwa maendeleo au tuiache bila ya kufanya kitu chochote. Hii ni nafasi ya kipekee kwa Msumbiji. Lakini marafiki zangu haki ya kupinga ni haki ya wananchi wa Msumbiji” alisema kiongozi huyo wa upinzani.

Matokeo rasmi yaliyotangazwa Jumatatu joini yanaongeza muda wa nusu karne kwa Frelimo kubaki madarakani na matayarisho kwa Chapo kuchukua madaraka kutoka kwa Rais Felipe Nyusi mwishoni mwa muhula wake wa pili hapo Januari 15.

Forum

XS
SM
MD
LG