Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 23:35

Ethiopia yasema marubani walijaribu kuiokoa ndege iliyouwa watu 157


Dagmawit Moges
Dagmawit Moges

Waziri wa uchukuzi wa Ethiopia Dagmawit Moges amesema Alhamisi kwamba marubani wa ndege iliyoanguka karibu na Addis Abbab Machi 10, na kusababisha vifo vya watu 157, walifuata taratibu zote katika kujaribu kuiokoa ndege aina ya Boeing 737 Max 8, lakini hawakufanikiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Addis Ababa Alhamisi bi Dagmawit, alisisitiza kwamba marubani walifuata utaratibu na kanuni zote waliokuwa wanazifahamu kujaribu kuiokoa ndege yao lakini hawakufanikiwa.

Dagmawit Moges, Waziri wa Uchukuzi wa Ethopia ameeleza : "Marubani walitekeleza utaratibu wote waliopewa na watengenezaji wa ndege mara kwa mara lakini hawakuweza kuidhibiti ndege hiyo. Marubani hao walipata leseni na mafunzo kuweza kuendesha ndege hiyo."

Zaidi ya hayo amesema serikali ya Ethiopia imetoa mapendekezo mawili juu ya usalama na kutaka chombo cha kuongoza ndege kuchunguzwa upya.

Na wachunguzi wa Ethopia pia wametoa ripoti yao ya awali juu ya ajali hiyo kufuatana na chombo cha kurikodi mawasiliano ya rubani na safari ya ndege inayofahamika kama Black Box, wakisisitiza pia kwamba marubani walifuata utaratibu unaotakiwa pindi tatizo linapotokea.

Dagmawit aliongeza kusema kwamba uchunguzi kamili utakamilika baada ya mwaka mmoja.

Wachunguzi wa upande wa Ethopia kuhusiana na ajali hiyo walizungumza pia na wandishi wa habari na kuthibitisha kile waziri alichosema lakini kuongeza kwamba hawawezi kuthibitisha kwa hivi sasa iwapo kulikuwa na tatizo la namna ya ndege hiyo ilivyotengenezwa au chombo chochote kilikuwa na hitilafu.

Ajali hiyo ya Machi 10 ilisababisha mashirika yote ya ndege duniani yanayotumia ndege hiyo ya 737 max 8 kupiga marufuku kwa muda utumiaji wa ndege hiyo na nchi kadhaa kupiga marufuku kuruka katika anga zao.

Tume ya wachunguzi 18 wa kimataifa wanaendelea na uchunguzi wao kwa muda wa miezi sita hadi mwaka mmoja ijayo.

Hapo Jumatano shirika la Boeing lilitangaza kwamba limefanya majaribio kutokana na marekebisho waliofanya katika chombo cha kuongoza ndege hiyo na wamefanikiwa.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Abdushakur Aboud, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG