Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 22, 2025 Local time: 18:43

Dunia yatakiwa kusimama pamoja katika kutatua mizozo


Rais wa Marekani Joe Biden akihutubia Mkutano wa 78th wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA, Majadiliano ya Jumla katika makao makuu ya UN, New York
Rais wa Marekani Joe Biden akihutubia Mkutano wa 78th wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA, Majadiliano ya Jumla katika makao makuu ya UN, New York

Viongozi wa dunia Jumanne wametoa mwito wa suluhisho la pamoja kushughulikia yanayo ikabili dunia kwa sasa kuanzia amani, mabadiliko ya hali ya hewa, demokrasia, na hali ya chakula katika siku ya kwanza ya hotuba za viongozi katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Akifungua mkutano wa 78, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonia Gutteres, ameyataka mataifa kuungana katika kutataua masuala mbalimbali ambayo yanahatarisha hali njema ya ulimwengu.

UN-ASSEMBLY/
UN-ASSEMBLY/

Amesema ili kufanikiwa kutatua masuala kama vile amani, na matatizo yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa, ni wajibu wa mataifa yote kufanyakazi kwa pamoja kwa ajili ya utatuzi wake.

Hotuba ya Gutteres ilikuwa ya ufunguzi wa hotuba kutoka kwa wakuu na viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.

Rais Baiden ahutubia mkutano mkuu wa Baraza Kuu la UM

Akihutubia hadhira ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na dunia, rais wa Marekani, Joe Biden, pia alitoa ujumbe kwa dunia kwenda pamoja kutatua changamoto za kidunia licha ya uwepo wa tofauti mbalimbali.

Pamoja na hilo, hotuba yake iligusia msimamo wa Marekani wa hali ya amani na ukiukwaji wa demokrasia barani Afrika.

Amesema taifa lake halitaacha kukemea kusambaa kwa uvunjwaji wa demokrasia na mapinduzi katika eneo la Sahel pamoja na ukanda wa Afrika Magharibi na Kati kwa ujumla.

Katika ajenda muhimu ya mabadiliko ya hali ya hewa, rais Joe Biden, amesema kwamba Marekani imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Amesema ili dunia kuwa salama, lazima ushiriki wa pamoja uwepo kuuokoa ulimwengu na majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa na kutolea mfano mafuriko ya Libya yaliyo sababisha vifo vya maelfu ya watu. Rais Biden pia alitoa pole kwa wale walioathirika na janga hilo.

Zelenskyy asisitiza Russia haipaswi kuaminiwa

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kikao cha 78, nchini Marekani.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kikao cha 78, nchini Marekani.

Katika hotuba yake ya kwanza wakati vita vya Ukraine na Russia vikiwa vinaendelea kwa zaidi ya mwaka, Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy amesema Russia haipaswi kuaminika katika matumizi ya silaha za nyuklia.

Katika hotuba yake ya mchana, akiwa amevalia fulana ikiwa ni ishara ya kuwa yupo vitani, rais Zelenskyy amesema kwamba, Russia haipaswi kuungwa mkono kwa namna yoyote na kufanya hivyo ni kukaribisha kusambaa kwa udhalimu duniani.

Rais Zelenksyy ambaye alikuwepo katika ukumbi wakati rais wa Marekani, Joe Biden anahutubia, amesema Russia haipaswi kuachiwa kuwa na silaha za nyuklia na matumizi yake. Ameisihi dunia kuunga mkono katika kuhakikisha uchokozi wa Russia, hauwi mfano kwa wengine.

Amesema endapo Russia, itapuuzwa, matendo yake yanaweza kusambaa mpaka maeneo mengine na kuhatarisha usalama wa dunia.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Idd Ligongo, New York, Marekani.

Forum

XS
SM
MD
LG