Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 22, 2025 Local time: 03:33

DRC: Papa Francis awasihi waliodhulumiwa kusamehe, awataka wamuige Yesu


Watu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wakimshangilia  Papa Francis alipoanza kuzunguka taratibu kwenye viwanja vya wazi  akiwa katika gari lake la kipapa mjini Kinshasa.
Watu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wakimshangilia  Papa Francis alipoanza kuzunguka taratibu kwenye viwanja vya wazi  akiwa katika gari lake la kipapa mjini Kinshasa.

Papa Francis Jumatano aliwasihi watu wa Kongo kuwasamehe wale walio wadhuru, alisema hayo alipokuwa  akiongoza misa iliyohudhuriwa  na watu takriban milioni moja...

Papa Francis Jumatano aliwasihi watu wa Kongo kuwasamehe wale walio wadhuru, alisema hayo alipokuwa akiongoza misa iliyohudhuriwa na watu takriban milioni moja waliofurika kuhudhuria tukio kubwa la kwanza la papa Francis barani Afrika lenye lengo la kuleta amani na maridhiano kwa nchi iliyoathiriwa na miongo kadhaa ya ghasia.

Waumini wengi wa Kongo walikesha wakisubiri misa kwenye viwanja vikubwa kwenye uwanja wa ndege wa Ndolo walisubiri kuwasili kwa papa Francis, wakiimba , kucheza na wakiwa wamejawa na msisimko juu ya ujio wa kwanza wa papa tangu Mtakatifu John Paul wa Pili alipofanya ziara yake ya mwisho mwaka 1985.

Walishangilia wakati Francis alipoanza kuzunguka taratibu kwenye viwanja vya wazi akiwa katika gari lake la kipapa. Baadhi yao wakikimbia kando yake au kupeperusha bendera. Wanawake wengi walikuwa wamevalia magauni na sketi zilizoshonwa kwa vitenge vya waksi vyenye picha ya papa Francis au alama nyingine za kidini.

"Leo ninaelewa shauku ya bibi yangu wakati Papa John Paul II alipokuja," alisema Julie Mbuyi, mama wa watoto wawili mwenye umri wa miaka 45, ambaye alikuwa amevalia mavazi yaliyokuwa na ujumbe wa Francis. "Alifurahi sana kumuona na usiku ule kabla ya kuwasili kwa papa hakuweza kulala!"

Papa Francis akutana na waumini wa Kanisa Katoliki nchini DRC.
Papa Francis akutana na waumini wa Kanisa Katoliki nchini DRC.

Umati wa watu ulishangilia tena wakati papa mwenye asili ya Argentina alipowasalimia kwa lugha ya Kilingala, moja wapo ya lugha nne za kitaifa za Kongo ambayo inazungumzwa na watu wengi katika mji mkuu wa Kinshasa. Na walisikiliza kwa makini alipokuwa akihubiri akiwasihi Wakongo kufungua mioyo yao ili wasamehe, alitoa mfano wa Yesu ambaye aliwasamehe wale waliomsaliti. “H

"Aliwaonyesha majeraha yake, kwa sababu msamaha huzaliwa kutokana na majeraha," Francis alisema. “Unazaliwa wakati majeraha yetu hayaachi makovu ya chuki, bali yanakuwa njia yakuwapa wengine nafasi na kukubali udhaifu wao. Udhaifu wetu unakuwa fursa, na msamaha unakuwa njia ya amani.”

Akielezea miongo kadhaa ya ghasia hasa mashariki mwa Kongo ambako imewalazimu mamilioni kukimbia makazi yao , Francis alisisitiza kusamehe hakumaanishi kujifanya kuwa hakuna kitu kibaya kilichotokea. Lakini alisema kitendo cha msamaha kinajenga "kuuacha moyo huru."

Manufaa makubwa tunayoyapata ni kusafisha mioyo yetu ya hasira na majuto ya kila aina ya chuki na uadui” alisema.

Misa ya asubuhi ilikuwa tukio kubwa la kwanza kwa papa Francis nchini Kongo baada ya kuwasili siku ya Jumanne na, katika hotuba yake ya ufunguzi kwa mamlaka za serikali, alilaani uporaji wa karne nyingi wa madini na maliasili ya Afrika unaofanywa na mataifa ya kigeni.

Mwisho--

XS
SM
MD
LG