Ziara ya Papa kuanzia Januari 31 hadi Februari 5 huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Sudan Kusini, inampeleka kiongozi huyo wa kanisa katoliki duniani mwenye umri wa miaka 86 hadi sehemu ambazo Wakatoliki ni takriban nusu ya wakazi wao na ambako Kanisa hilo ni mdau muhimu katika afya na mifumo ya elimu pamoja na juhudi za kujenga demokrasia.
Ziara hiyo ilipangwa kufanyika Julai mwaka jana lakini iliahirishwa kwa sababu Francis alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya muda mrefu ya goti. Bado anatumia kiti cha magurudumu na fimbo lakini goti lake limeimarika sana.
Nchi zote mbili zina utajiri mkubwa wa maliasili - DRC katika madini na Sudan Kusini katika mafuta lakini zinakabiliwa na umaskini na migogoro.
DRC, ambayo ni nchi ya pili kwa ukubwa barani Afrika na ina wakazi wapatao milioni 90, inapata ziara yake ya kwanza ya Papa tangu John Paul II alipolitembelea taifa hilo mwaka 1985, wakati ilipokuwa ikijulikana kama Zaire.