Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Desemba 22, 2024 Local time: 14:44

Daktari Abu-Sittah aelezea kuzorota kwa huduma za afya katika hospitali ya Shifa, Gaza


Daktari Sidhat Saidam aliyeuawa pamoja na familia yake.
Daktari Sidhat Saidam aliyeuawa pamoja na familia yake.

Ghassan Abu-Sittah, daktari bingwa wa upasuaji raia wa Uingereza mwenye asili ya Palestina, wa shirika la  Madaktari Wasio na Mipaka (Doctors Without Borders) alizungumza na Sauti ya Amerika kutoka Hospitali ya Shifa huko Gaza:

"Naitwa Dr. Ghassan Abu-Sittah, mimi ni daktari wa upasuaji wa kurekebisha viungo na ngozi na ninafanya kazi na MSF. Kwa sasa nipo hospitali ya Shifa, na hali hapa ni ya kusikitisha sana. Kuna janga la afya ya umma.

Kuna maelfu, ikiwa si dazeni za maelfu ya watu ambao wametafuta hifadhi hospitalini, wamelala kwenye sakafu, lakini pia ndani ya hospitali, kwenye ngazi, kwenye korido, na katika wodi, katikati ya vitanda vya wagonjwa.

Unajua hali ya usafi si nzuri kwa sababu ya ukosefu wa maji, na hakuna fursa ya kuyapata maji.

Watu hawa wana hofu kubwa ya mlipuko wa bomu, inaeleweka ni kwa nini.

Leo, daktari bingwa wa upasuaji kutoka Hospitali ya Shifa ambaye alikuwa ametoka kwenye zamu yake na kwenda kuiangalia familia yake aliuawa pamoja na watu 30 wa familia yake. Alikuwa anaitwa Sidhat Saidam.

Na siyo yeye peke yake. Idadi ya wafanyakazi inapungua kwa sababu ya ukweli kwamba baadhi ya watu hawawezi tena kufika hospitali kwa usalama.

Baadhi ya watu wameamua kuwa wanahitaji kuwa na familia zao. Watu wengine wamepoteza familia na watu wengine wameuawa.

Na hivyo, vyumba vya upasuaji havifanyi kazi.

Waisraeli wanajaribu kulazimisha kufungwa kwa hospitali nyingi, haswa kaskazini, na wamewataka wakurugenzi wa hospitali na kutishia kuzilenga hospitali hizi ili kulazimisha zifungwe.

Waisraeli wanajaribu kulazimisha kuporomoka kwa mfumo wa afya kama sehemu ya shinikizo kwa jamii ya Wapalestina.

Kuna zaidi ya wagonjwa 150 ambao wanahitaji kufanyiwa upasuaji na hawawezi.

Sasa tunaona matokeo ya kuchelewesha upasuaji kwa wagonjwa ambao hawajaweza kwenda kwenye chumba cha upasuaji.

Wenzangu walilazimika kurekebisha uso wa mtu kwa kutumia ganzi ya kiasili kwa sababu hakuna jinsi ya kuingia katika chumba cha upasuaji, kwa sababu vyumba vyote vilivyopo vimejaa na watoa dawa ya ganzi walikuwa na shughuli nyingi.

Bidhaa zimekuwa adimu. Kuna upungufu wa maji na chakula ni kidogo.

Mpaka jumuiya ya kibinadamu itakapoingilia kati.

Hadi kutakapokuwa na njia kwa misaada ya kibinadamu ili kusambaza bidhaa na vifaa vya hospitali na kuwaondoa waliojeruhiwa.

Mpaka pale kutakapokuwa na sitisho la mashambulizi, basi eneo hili linaelekea kuwa katika janga kubwa.”

Forum

XS
SM
MD
LG