“Tuna mengi ya kuzungumza. Nafikiri tunafanya vizuri. Tunaendelea kwenye njia ambayo ni chanya,” alisema Biden.
“Ni vyema kwetu kuendelea na mazungumzo, ambayo tulikuwa nayo mwezi mmoja au zaidi uliopita, tunahisi kama tuko White House, ambako tulisaini Azimio la Atlantic,” alisema Sunak, akiuelezea mkataba wa Juni wa kushirikiana katika teknolojia ya juu, nishati safi, na madini muhimu kukabiliana na China katika ushawishi wake ulimwenguni.
Maafisa wa utawala wa Biden wamesisitiza kuwa hii ni ziara ya sita ya viongozi hao katika kipindi cha miezi sita.
Hata hivyo, mkutano huo umeghubikwa na tangazo la hivi karibuni la Washington kuwa itapeleka mabomu yanayolipua mabou mengine huko Ukraine, licha ya kuwa mabomu hayo yamepigwa marufuku na nchi 123, ikiwemo Uingereza, kwa sababu ya uwezo wa mabomu hayo kuua kiholela.
Sunak hajaunga mkono hadharani hatua hiyo, akieleza siku ya Jumamosi kuwa Uingereza imesaini azimio linalopiga marufuku utengenezaji au matumizi ya mabomu hayo na inashawishi kutokutumiwa.
“Tutaendelea kwa upande wetu kuisaidia Ukraine dhidi ya uvamizi haramu na bila ya uchokozi uliofanywa na Russia, lakini tumefanya hivyo kwa kutoa vifaru imara vya kivita na hivi karibuni silaha za masafa marefu, na tunatumai nchi zote zitaendelea kuiunga mkono Ukraine,” aliwaambia waandishi wa habari.
Sunak alikuwa anatekeleza “jukumu lake la kisheria” kwa mujibu mkataba unaojulikana kama ‘Convention on Cluster Munitions’, mshauri wa Usalama wa Taifa wa White House Jake Sullivan aliwaambia waandishi wa habari akiwa katika ndege ya Air Force One siku ya Jumapili.
Alikanusha kuwa dhana ya uamuzi wa kupeleka mabomu ulikuwa unaleta mgawanyiko katika muungano.
“Nafikiri utagundua Waziri Mkuu Sunak na Rais Biden wako katika msimamo mmoja wa kimkakati juu ya Ukraine, wakichukua hatua ya pamoja kuangalia picha kubwa zaidi ya kile wanachotaka kukifanikisha, wakiwa wameungana kama ilivyo kawaida katika mgogoro huu na liko wazi,” alisema.
Biden na Sunak wanalenga pia kutafuta njia sahihi ya kuhakikisha usalama wa muda mrefu wa Kyiv ikiwa nje ya muundo wa NATO wakati Kyiv ikipiga hatua kuwa mwanachama.
Biden amesema haamini kuwa Ukraine iko tayari kujiunga na muungano huo, akitaja mageuzi yanayohitajika na hatari ya kuitumbukiza NATO katika mgogoro wa moja kwa moja na Russia.
Chanzo cha habari hii ni mashirika ya habari ya AP, na AFP.
Forum