Rais wa Marekani Joe Biden aliwasili mjini London Jumapili kwa ziara ya siku tano barani Ulaya, akianzia Uingereza. Kisha atasafiri kwenda Lithuania kwa mkutano wa NATO huko Vilnius, kabla ya kusimama katika kituo cha mwisho nchini Finland kukutana na viongozi wa Nordic.
Mjini London, Biden atakuwa na mikutano na Waziri Mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak na Mfalme Charles kujadili masuala mbalimbali ya nchi hizo mbili na ufadhili wa hali ya hewa kwa mataifa yanayoendelea. Mwezi mmoja uliopita, huko Washington, Biden na Sunak walikubaliana kwa “Azimio la Atlantic” na kushirikiana katika teknolojia za hali ya juu, nishati safi, pamoja na madini muhimu.
Rais Biden alikuwa mwenyeji wa Sunak huko White House. Katika mkutano wa kilele wa NATO, viongozi wa nchi za Magharibi watajadili juhudi zao za hivi karibuni za kuimarisha mapambano ya Ukraine dhidi ya Russia pamoja na jitihada za Sweden kujiunga na muungano mkuu wa kijeshi wa nchi za Magharibi.
Forum