Mzozo wa silaha umepamba moto huko Myanmar katika jimbo la kaskazini la Shan tangu Oktoba, wakati ushirika wa vikundi vya kikabila vya walio wachache vilipoanzisha mashambulizi dhidi ya utawala wa kijeshi.
Vyombo kadhaa vya habari vya China viliripoti Jumatano kuwa mashambulizi ya makombora kutoka Myanmar yalianguka upande wa pili wa mpaka kwenye mji wa Nansan katika jimbo la Yunnan nchini China, ambako yalilipuka na kusababisha watu mbalimbali kujeruhiwa.
Shirika la habari la AFP halikuweza kupata uthibitisho huru wa ripoti hizo au picha zilizoambatana zilizobandikwa katika mitandao ya kijamii.
Alipoulizwa kuhusu ripoti hizo katika mkutano wa kawaida wa waandishi wa habari Alhamisi, msemaji wa wizara ya mambo ya nje Wang Wenbin alisema China “inaelezea kutoridhishwa vikali na hali ya mgogoro huo wa kivita uliosababisha vifo vya raia wa China,” akiongeza kuwa Beijing “ilipeleka uwakilishi mzito kwa pande zote husika.
China kwa mara nyingine imedai kuwa pande zote za mgogoro wa kivita ulioko kaskazini mwa Myanmar usitishe mapigano hayo mara moja na kuchukua hatua thabiti kuzuia matukio maovu kuendelea kutokea ambayo yanahatarisha usalama na utulivu katika mpaka huo,” Wang alisema.
“China itachukua hatua zote muhimu kulinda usalama wa maisha ya raia wake na mali zao,” alisema.
Wang hakufafanua ni watu wangapi walikuwa wameuawa au kujeruhiwa katika tukio hilo.
Ushirika wa kikabila umekamata miji kadhaa na vituo vya mpakani muhimu kwa biashara na China kwa kile wachambuzi wanachosema ni changamoto kubwa sana ya kijeshi kwa utawala wa kijeshi tangu ulipochukua madaraka 2021.
Mwezi uliopita, Beijing ilisema ilikuwa imesimamia mazungumzo kati ya jeshi la Myanmar na vikundi venye sialaha vya ushirika wa kikabila na kufikia makubaliano “ sitisho la muda la mapigano.”
Hata hivyo, mapambano yameendelea katika baadhi ya sehemu za jimbo la Shan, na ubalozi wa China wiki iliyopita uliwataka raia wake kuondoka katika eneo hilo lilioko kwenye mpaka wanaoshirikiana kutokana na hatari za kiusalama.
Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la AFP.
Forum