Gari lililokuwa limejaa vilipuzi liligonga kwenye nyumba ya wageni iliyokuwa inawahudumia maafisa wa serikali katika jiji la Bardera, kiasi cha kilomita 450 magharibi mwa mji mkuu wa Mogadishu, alisema kamanda wa polisi wa eneo hilo Hussein Adan.
"Mlipuko huo uliharibu sehemu kubwa ya jengo hilo na kuua walinzi watano,"kamanda wa polisi aliliambia shirika la habari la AFP.
Watu wengine 11, akiwemo gavana Ahmed Bulle Gared, walijeruhiwa, aliongeza.
Al-Shabaab, yenye uhusiano na la Al-Qaeda, kwa takriban miaka 15 imekuwa ikifanya uasi wa kijihadi wa umwagaji damu dhidi ya serikali kuu katika taifa hilo tete lililoko katika Pembe ya Afrika.
Kundi la Al-Shabaab limedai kuhusika na shambulio hilo kupitia Shirika lao la Habari la Shahada, kulingana na taarifa ya kundi la ufuatiliaji la Marekani, SITE.
Mohamud Saney, ambaye alishuhudia shambulio la Jumanne, alisema "hajawahi kusikia mlipuko mkubwa kama huo."
"Ulioitikisa ardhi kama tetemeko la ardhi."
Katika shambulio baya zaidi la Al-Shabaab tangu kuanza mashambulizi haya mwaka jana, watu 121 waliuawa mwezi Oktoba katika milipuko miwili ya mabomu yaliyotegwa kwenye gari kwenye eneo la wizara ya elimu mjini Mogadishu.
Katika miezi ya hivi karibuni, jeshi la Somalia na wanamgambo wa koo za eneo hilo wamechukua tena udhibiti wa sehemu kadhaa za maeneo yaliyokuwa yametekwa na wanamgambo hao katika operesheni iliyoungwa mkono na mashambulizi ya anga ya Marekani na kikosi cha Umoja wa Afrika kinachojulikana kama ATMIS.
Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la AFP