Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud leo Jumatano alikuwa mwenyeji wa mkutano wa viongozi kutoka nchi kadhaa jirani kujadili mapambano dhidi ya al-Shabaab wakati mashambulizi mapana dhidi ya wanamgambo hao yakishika kasi.
Mkutano huo unaofanyika katika mji mkuu Mogadishu unawakutanisha viongozi kutoka "nchi tatu jirani", ofisi ya Rais wa Somalia ilisema, ikibandika picha za kuwasili kwa William Ruto wa Kenya, Ismail Omar Guelleh wa Djibouti na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed.
Wanatarajiwa kujadili uratibu wa mashambulizi ya kijeshi dhidi ya kundi linalohusishwa na al-Qaeda ambalo limekuwa likifanya uasi katika taifa hilo lenye matatizo la Pembe ya Afrika kwa zaidi ya miaka 15.
Usalama uliimarishwa mjini humo, doria za kijeshi na safari zote za ndege za kibiashara zilisitishwa.
"Barabara kuu na mitaa mjini humo imefungwa hivi leo na hakuna vuguvugu la raia linaloruhusiwa," Abdulahi Hassan, wa idara ya usalama wa taifa, alisema.