Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 22, 2025 Local time: 22:15

Afrika Kusini: Viongozi wa jumuiya ya BRICS wajadili kanuni za kuwaleta wanachama wapya katika umoja huo


Kutoka kushoto: Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva, Rais wa China Xi Jinping, Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov, wakikutana Afrika Kusini, Agosti 23, 2023. REUTERS/Alet Pretorius/Pool
Kutoka kushoto: Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva, Rais wa China Xi Jinping, Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov, wakikutana Afrika Kusini, Agosti 23, 2023. REUTERS/Alet Pretorius/Pool

Viongozi wa BRICS wamekuwa wakijadili kanuni za kuwaingiza wanachama wapya katika umoja huo wa nchi zinazoendelea  katika mkutano wa leo Jumatano wakati kuna migawanyiko juu ya mustakbali wa mwelekeo ambao unaweza kudumaza utashi wake wa kuupa nguvu zaidi umoja huu  katika masuala ya kimataifa.

Mataifa yenye nguvu katika Umoja huo China na Russia – ambayo rais wake Vladimir Putin anahudhuria kwa njia ya mtandao wanataka kuiimarisha BRICS huku kukiwa na mivutano mikubwa ikiwa ni matokeo ya vita vya Ukraine na ushindani unaozidi kukua kati ya Beijing na Washington.

Rais wa Russia Vladimir Putin ameuambia mkutano kwamba Russia ilitaka kumaliza vita alivyosema “vimesababishwa na Magharibi na satalaiti zake” nchini Ukraine.

Akiongea kwa njia ya video na viongozi wa kundi hilo, ambao wamejiweka kando kushutumu hatua za Moscow nchini Ukraine, alirejea maelezo ambayo yamekuwa yakitolewa na Kremlin kwamba vita ilikuwa ni majibu kwa hatua zilizochukuliwa na Kyiv na Magharibi.

Rais Putin anasema “hatua zetu nchini Ukraine zimeshawishiwa na sababu moja tu – kumaliza vita, ambavyo vimeletwa na Ukraine na magharibi na satalaiti zao dhidi ya watu ambao wanaishi katika Mkoa wa Donbas. Tunawashukuru washirika wenzetu katika BRICS ambao kwa bidi wameshiriki katika majaribio ya kumaliza hali hii na kufikia suluhisho la haki kwa njia ya amani.”

Uchumi wa Russia unasua sua kwasababu ya vikwazo vya Magharibi kutokana na vita vya Moscow nchini Ukraine. Putin anatafutwa kwa mujibu wa hati ya kimataifa kwa shutuma za uhalifu wa vita nchini Ukraine na anawakilishwa katika mkutano huu na waziri wake wa mambo ya nje, Sergei Lavrov.

Wakati huo huo Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, aliwaambia wajumbe kwamba umoja huo utaendelea na majadiliano kuhusu matumizi ya sarafu za ndani ili kufanikisha mtiririko wa biashara na uwekezaji.

Rais wa Russia Vladimir Putin (Kulia) akishiriki katika mkutano wa Jumuiya ya BRICS kwa njia ya mtandao. Anamsikiliza Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa (kushoto) akihutubia mkutano huo.(Mikhail Klimentyev, Sputnik, Kremlin Pool Photo via AP)
Rais wa Russia Vladimir Putin (Kulia) akishiriki katika mkutano wa Jumuiya ya BRICS kwa njia ya mtandao. Anamsikiliza Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa (kushoto) akihutubia mkutano huo.(Mikhail Klimentyev, Sputnik, Kremlin Pool Photo via AP)

“Tuna wasi wasi kwamba mifumo ya fedha na malipo ya kimataifa inazidi kutumiwa kama nyenzo inayogombaniwa kisiasa na kijiografia. Kufufuka kwa uchumi wa ulimwengu kunategemea mifumo ya uhakika ya kimatiafa ya malipo na mwenendo mzuri wa kibenki, mfumo wa usambazaji na biashara, utalii pamoja na mtiririko wa kifedha. Tutaendelea na majadiliano kuhusu hatua muafaka kufanikisha mifumo ya biashara na uwekezaji kupitia kuongeza matumizi ya sarafu za ndani,” anasema Rais Ramaphosa.

BRICS, ni umoja unaoibuka ambao wanachama wake ni Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini nchi zenye takribani asilimia 40 ya idadi ya watu ulimwenguni na kiasi cha asilimia 25 ya uchumi wa dunia.

Zaidi ya nchi 20 zimeomba rasmi kujiunga na kundi hilo, maafisa wanasema ikiwemo Saudi Arabia moja ya nchi muhimu sana.

Akiongea na waandishi wa habari hapa Washington siku ya Jumanne, mshauri wa usalama wa taifa Jake Sullivan alisema haioni BRICS kugeuka kuwa mshindani wa Marekani.

Forum

XS
SM
MD
LG