Viongozi wa mataifa ya BRICS - Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini wamekutana mjini Johannesburg siku ya Jumanne kwa ajili ya mkutano wao ambapo watapima uzito wa kuupanua umoja huo huku baadhi ya wanachama wakishinikiza kuingia katika mapambano dhidi ya nchi za Magharibi.
Kuongezeka kwa mivutano ya kimataifa iliyochochewa na vita vya Ukraine na kuongezeka kwa ushindani kati ya China na Marekani kumeongeza uharaka katika harakati za kuimarisha umoja huo ambao wakati fulani umekumbwa na migawanyiko ya ndani na ukosefu wa mtizamo madhubuti.
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alimkaribisha Rais Xi Jinping wa China mtetezi mkuu wa kuongeza ukubwa wa BRICS kwenye ziara ya kiserikali Jumanne asubuhi kabla ya kukutana na viongozi wengine wa kundi hilo baadaye mchana.
Rais Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi pia wanahudhuria mkutano huo wa Agosti 22 hadi 24.
Rais wa Russia Vladimir Putin anayetakiwa na mahakama ya kimataifa baada ya kutolewa ya kukamatwa kwa madai ya uhalifu wa kivita nchini Ukraine hatakwenda Afrika Kusini na badala yake atajiunga nao kwa njia ya mtandao.
Forum