Youssouf alishinda nafasi hiyo baada ya kuwabwaga wagombea wengine wawili: Raila Odinga, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, na Richard Randriamandrato, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Madagascar.
Youssouf atahudumu kwa kipindi cha miaka minne, akichukua nafasi ya Moussa Faki wa Chad, ambaye amekuwa akishikilia wadhifa huo tangu mwaka 2017.
Youssouf amekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti tangu mwaka 2005, na kabla ya hapo alihudumu kama balozi wa nchi hiyo nchini Misri.
Uzoefu wake wa muda mrefu katika diplomasia na uongozi ulimpa nafasi nzuri ya kushinda uchaguzi huo muhimu, kwa mujibu wa wachambuzi wa siasa.
Kuchaguliwa kwake kunajiri wakati ambapo Umoja wa Afrika unakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwa ni pamoja na hofu ya vita nchini Kongo kugeuka kuwa mgogoro wa kikanda.
Raila Odinga, mwenye umri wa miaka 80, ni mwanasiasa mashuhuri nchini Kenya ambaye amewania urais mara tano katika kipindi cha miongo mitatu.
Kwa wakati mmoja alielezea matumaini kwamba nafasi ya uenyekiti wa AUC ingekuwa mchango wake wa mwisho katika utumishi wa umma.
Kama Mwenyekiti mpya wa Tume ya Umoja wa Afrika, Youssouf anakabiliwa na changamoto mbalimbali, zikiwemo kuongezeka kwa utawala wa kijeshi katika nchi za Afrika Magharibi na uasi unaoendelea katika eneo la mashariki mwa Kongo.
Katika siku za hivi karibuni, waasi wanaoungwa mkono na Rwanda wamechukua udhibiti wa miji miwili muhimu katika eneo hilo, hali inayoongeza wasiwasi wa usalama na utulivu katika kanda hiyo.
Umoja wa Afrika umekuwa ukikosolewa mara kwa mara kwa kile kinachoonekana kama kutokuchukua hatua madhubuti au kukosa mwitikio wa haraka katika kukabiliana na migogoro ya kivita katika sehemu mbalimbali za bara la Afrika.
Kuchaguliwa kwa Youssouf kunaleta matumaini mapya ya uongozi thabiti na hatua za haraka katika kushughulikia changamoto hizi zinazolikabili bara, kwa mujinbu wa wachambuzi.
Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa kijamii wa X, Waziri wa Uchumi na Fedha wa Djibouti, Ilyas Dawaleh, alithibitisha ushindi wa Youssouf kwa kusema kwamba alikuwa ameshinda.
"Kuchaguliwa kwa Youssouf kunatoa fursa kwa Djibouti kuwa na ushawishi mkubwa zaidi katika masuala ya bara la Afrika, na pia kunampa jukumu zito la kuhakikisha kwamba Umoja wa Afrika unakuwa na sauti moja katika kushughulikia masuala muhimu yanayolikabili bara hili," alisema mchambuzi mmoja wa siasa za kikanda ambaye hakutaka jina lake litajwe.
"Wakati uongozi wake ukianza, matarajio ni kwamba atachukua hatua madhubuti katika kushughulikia migogoro na kukuza maendeleo endelevu katika nchi wanachama wa Umoja wa Afrika," aliongeza.
Forum