Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 30, 2025 Local time: 05:01

Yanayojiri Goma, DRC


Wanajeshi wa DRC wakishika doria nje ya mji wa Goma, DRC. Waasi wa M23 wanapigana na wanajeshi wa DRC ndani ya Goma
Wanajeshi wa DRC wakishika doria nje ya mji wa Goma, DRC. Waasi wa M23 wanapigana na wanajeshi wa DRC ndani ya Goma

Mapigano makali yanaendelea kati ya wanajeshi wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na wapiganaji wa kundi la waasi la M23 wanaoungwa mkono na wanajeshi wa Rwanda, katika mji wa Goma.

Kuna ripoti za miili ya watu kutapakaa barabarani.

Hospitali zimejaa majeruhi wa vita hivyo.

Katika mji mkuu wa Kinshasa, waandamanaji wanaolalamikia ukosefu wa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua, wameshambulia balozi za Rwanda, Ufaransa, Ubelgiji, Marekani, Uganda, Kenya na Afrika kusini.

Waasi wa M23, ambao umoja wa mataifa unasema wanaunga mkono na Rwanda, waliingia katika mji wa Goma mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, hatua ambayo ni pigo kubwa kwa jeshi la DRC kulinda mji huo na dhihirisho na kuongezeka kwa uhasama kati ya DRC na Rwanda.

Mamia ya watu wameuawa na mamilioni kukoseshwa makao.

'Jeshi la DRC linadhibithi 80% Goma'

Waziri wa maendeleo ya mitaani wa DRC Muhindo Nzangi amesema jeshi la DRC linadhibithi asilimia 80 ya Goma.

Rwanda iliripoti jana Jumatatu kwamba mabomu yalikuwa yakirushwa Kwenda Rwanda kutoka DRC. Rwanda imesema raia 5 waliripotiwa kuaawa na 25 kujeruhiwa.

Baadhi ya wanajeshi wa DRC pia waliripotiwa kukimbia vita na kuingia Rwanda ambapo walipokonywa silaha na kuwekwa chini ya ulinzi.

Umoja wa mataifa na mashirika mengine ya kutoa misaada wameonya kwamba hospitali katika mji wa Goma zimejaa watu waliojeruhiwa kwa risasi.

Vifo, majeruhi

Hadi wakati tunaandaa ripoti hii, mashirika ya kijamii yanasema watu 25 wamethibitishwa kuuawa, watu 375 wanatibiwa majeruhi ya risasi.

Shirika la chakula duniani WFP limesema kwamba shughuli za kutoa msaada wa chakula mjini Goma zimesitishwa kutokana na ukosefu wa usalama.

Mwandishi wa VOA Austere Malivika amesema huduma za umeme zimekatika mjini Goma na kuna uhaba wa chakula na mahitaji muhimu.

Afrika kusini imesema wanajeshi wake 13 wameuawa.

Mazungumzo kati ya Ramaphosa na Kagame

Rais wa Afrika kusini Cyril Ramaphosa amefanya mazungumzo na rais wa Rwanda Paul Kagame kwa njia ya simu na taarifa iliyotolewa baadaye inasema wawili hao wamekubaliana kuhakikisha kwamba vita vinasitishwa. Hakuna maelezo zaidi yametolewa.

Umoja wa Afrika unatarajiwa kuandaa kikao cha dharura kuhusu DRC hii leo huku marais wa jumuiya ya Afrika mashariki wakikutana kesho jumatatu ambapo rais wa DRC Felix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame wanatarajiwa kuhudhuria.

Kundi la M23

Kundi la M23, wengi wao kutoka kabila la Watutsi, linadai kupigania haki zao. Kundi hilo liliundwa mwaka 2012 baada ya baadhi ya wanajeshi wa serikali ya DRC, kuasi wakidai kwamba walikuwa hawapati haki sawa katika jeshi.

Kundi la M23 liliwahi kudhibithi mji wa Goma mwaka 2012 lakini wakafurushwa na jeshi la DRC likisaidiwa na walinda amani wa umoja wa mataifa. M23 walikimbia na kujifichwa katika milima iliyo karibu na Rwanda mwaka 2013.

Shutuma dhidi ya Rwanda

Umoja wa mataifa unashutumu Rwanda, kwa kuunga kundi la M23, ikiwa Pamoja na kutuma wanajeshi wa Rwanda kusaidia waasi hao.

Rwanda pia inashutumiwa kwa kutoa silaha na mafunzo kwa M23. Rwanda imekuwa ikikanusha madai hayo na kudai kwamba DRC inaunga mkono kundi la waasi la Democratic forces for the liberation of Rwanda FDLR linaloshutumiwa kwa kusababisha mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda.

Baraza la usalama la umoja wa mataifa linakutana baadaye hii leo Jumanne kujadili hali ya usalama mashariki mwa DRC.

Forum

XS
SM
MD
LG