Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani Tedros Adhanom Ghebreyesus anasema kuna kazi kubwa inayohitajika kupambana na janga la virusi vya corona licha ya kuwepo na habari nzuri wiki hii kuhusiana na mafanikio ya majaribio ya chanjo.
Akizungumza kutoka Geneva Ijumaa wakati idadi ya maambukizo yakiwa yameongezeka kote duniani Tedros amesema chanjo ni chombo kimoja tu katika kupambana na janga hili lakini watu wasisahau masharti mengine ya kujikinga Ikiwa tunataka kutokomeza ugonjwa huu.
Idadi ya watu wanaoambukizwa kwa siku huko Rushia na Marekani zimefikia kiwango cha juu kuwahi kushuhudiwa tangu janga hili kuanza.
Rashia iliripoti kuwepo na zaidi ya watu 21,000 walioambukizwa jana pekee yake.
Huko Ulaya hali ya wasiwasi imezuka kutokana na kuongezeka maambukizo na kusababisha mataifa mengi kuanza kuchukua tena hatua kali za kudhibiti kuenea kwa virusi.
Huko ufaransa peke yake zaidi ya watu 35,000 waliambukizwa kwa kipindi cha saa 24 zilizopita.