WFP yasitisha mgao wa chakula kwa familia 700 Malawi

Mbali na kutoa msaada wa chakula, WFP imeendelea continues kutoa misaada ya vitu vingine kama mahema kwa walioathiriwa na mafuriko Malawi.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) nchini Malawi limesitisha mgao wa chakula kwa takriban familia 700 za wakimbizi, wakisema familia zilikuwa zinajikimu zenyewe.

Lakini wengi ambao wameondolewa kwenye orodha wanasema wanategemea mgao wa kila mwezi na kudai kuwa mchakato wa tathmini ulikuwa na dosari.

Mapendo Neema, na watoto wake saba, na mume ambaye hana kazi wamekuwa wakitegemea mgao wa chakula wa kila mwezi kwenye kambi ya wakimbizi ya Dzaleka nchini Malawi tangu mwaka 2016.

Walikimbia shambulizi la uasi huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, anasema yeye ni manusura wa ubakaji na wazazi walifariki.

Lakini mapema mwezi huu WFP iliziondoa familia yake na watu wengine takriban 700 katika kambi hiyo kwenye orodha ya wakimbizi ambao wanapatiwa msaada wa chakula.

Uamuzi huo ulimuacha Neema na familia yake wakijitahidi kujikimu kimaisha.

Huku machozi yakimtoka, Neema anasema, “watoto hawa hawajakula chochote tangu asubuhi kwa sababu hakuna chakula. Unadhani utapata wapi chakula cha kuwalisha wakati hakuna mgao ambao tunapokea kutoka WFP?” Ameongezea “nahisi kama familia yangu inazikwa ikiwa hai, kweli.”

Aliyeondolewa pia katika orodha hiyo ni Ramazani Tabu mwenye umri wa miaka 75, ambaye aliishi katika kambi tangu mwaka 2007 na kamwe hawezi tena kufanya kazi kuisaidia familia yake ya watu wanne.

Anasema, “nilipokuja hapa, nilikuwa na uwezo wa kushona kwasababu hiyo ndiyo kazi niliyokuwa naifanya nchini DRC. Lakini na utu uzima na hali yangu ya kisukari siwezi tena kushona nguo, kwasababu kila ninapokaa kwenye cherehani natoka damu za pua kutokana na shinikizo la damu.”

WFP inasema imelazimika kuziondoa familia katika mgao wa chakula baada ya kufanya tathmini mwaka 2020.

Mkurugenzi wa Kanda Paul Turnbull anasema viwango vya ufadhili na kuongezeka kwa idadi ya wakimbizi kumewalazimisha kulenga wale tu walio katika mazingira hatarishi.

“Kuna wakimbizi wengi hapa nchini Malawi ambao wamekuwepo hapa kwa muda mrefu. Wametafuta njia za kujikimu kimaisha. Kwahiyo, tumefanya, tathmini na tumebaini kundi la wale watu ambao wana shida ya usalama wa chakula na watu wale ambao hawana,” amesema Turnbull.

Lakini baadhi yao ambao wameondolewa katika orodha wanadai kuwa mchakato wa tathmini ulikuwa na mapungufu kwasababu zaidi ya nusu ya walioondolewa kutoka katika mgao wa chakula ni maskini na hawana kazi.

Raphael Ndabaga, mkimbizi kutoka DRC ni miongoni mwao.

“Sawa, mimi kama nilivyo unaiona hii nyumba ninayoishi. Simenti imebanduka, sina fedha. Siwezi kununua simenti, nahitaji fedha pia kwa ajili ya chakula cha watoto wangu,” anasema Ndabaga.

Turnbull anasema shirika la Umoja wa Mataifa la chakula hivi punde litaanza kusikiliza maombi kutoka kwa wale ambao wanaamini wameondolewa kimakosa kwenye mgao wa chakula.

“Kuna baadhi ya masharti ambayo tunayo kulingana na mazingira ya kiuchumi; mabadiliko katika mhimili wa kuhudumia familia; mambo kama hayo yatatumika kuamua iwapo watu warejeshwe katika orodha au la.”

Maafisa wa WFP wanasema wakimbizi waliondolewa katika mgao wa chakula bado wanaweza kupata msaada ambao si wa chakula katika kambi, kama vile fursa ya huduma zaz fya na fursa ya makazi.