Austin alilakiwa katika kituo cha treni mjini Kyiv na balozi wa Marekani nchini Ukraine, Bridget Brink, na mwambata wa kijeshi wa Marekani, Brigedia Jenerali Kipling Kahler, na aliyejiunga katika ziara hiyo ni Jenerali wa Marekani Christopher Cavoli, ambaye anahudumu kama Kamanda Mkuu wa Muungano wa NATO Ulaya, na mkuu wa Kamandi ya Marekani Ulaya.
Maafisa wakuu wa ulinzi wa Merekani walisema Austin alikuja Kyiv kujadili mapambano ya dharura ya msimu wa baridi na kupanga misaada wa kiusalama kwa siku zijazo.
Ni ziara ya kwanza ya Austin tangu mwezi Aprili 2022, imekuja wakati msimu wa baridi unaanza na ambapo maafisa wa Ukraine na Magharibi wana imani kuwa Rais wa Russia Vladimir Putin ataanza tena kulenga miundo mbinu muhimu kama alivyofanya msimu uliopita wa baridi, na kuwaacha Waukraine wengi bila nishati kwa siku kadhaa za mwaka huo zilizokuwa na baridi zaidi.
"Moja ya kitu muhimu zaidi cha kufanya katika msimu huu wa baridi itakuwa ulinzi wa anga," afisa mkuu wa pili wa ulinzi aliwaambia waandishi wa habari wanaosafiri na Austin, na kuzungumza kwa masharti ya kutotajwa jina.
Mashambulizi ya takriban ndege zisizokuwa na rubani 40 zilizotengenezwa na Iran zilizorushwa kutoka eneo la Russia zilishambulia ulinzi wa anga wa Ukraine mwishoni mwa wiki.
Ukraine ilisema kuwa vikosi vyake viliharibu ndege 29 kati ya 38, lakini zile zilizofanikiwa kupitia ulinzi wa Ukraine ziliipiga miundombinu na kusababisha kukatika kwa umeme katika miji na vijiji zaidi ya 400 vya maeneo mbalimbali ya nchi.
Ndege hizo zisizo na rubani zilishambulia kuanzia mikoa ya Odesa na Zaporizhzhia kusini, hadi eneo la Chernihiv kaskazini, karibu na mpaka na Belarus.
Pia wameilenga Kyiv katika shambulio la pili hadi sasa kwa mwezi huu, lakini ndege zote zisizo na rubani zilizokuwa zikielekea katika mji mkuu zilitunguliwa, maafisa wa Ukraine walisema.