Maafisa hao wawili walibadilishana mawazo kuhusu masuala mbalimbali yenye utata, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa mvutano katika Mlango-Bahari wa Taiwan, makabiliano yanayoendelea kati ya Ufilipino na China, katika Bahari ya South China, pamoja na migogoro mikubwa ya kimataifa kama vile vita vya Russia nchini Ukraine na mzozo wa Mashariki ya Kati.
Wakati wa mkutano huo wa dakika 75, Austin na Dong wote waliangazia umuhimu wa kudumisha njia wazi za mawasiliano kati ya majeshi ya nchi hizo mbili, na kuapa kurejesha njia ya kuwasiliana kwa dharura kati ya makamanda kutoka pande zote mbili katika miezi ijayo.
Austin alisisitiza wasiwasi wa Washington kuhusu mazoezi ya kijeshi ya siku mbili ya hivi karibuni ya China kuzunguka Taiwan na kuitaka Beijing kutotumia mabadiliko ya kisiasa ya Taiwan, ambayo aliyataja kama sehemu ya mchakato wa kawaida wa kidemokrasia, kama "kisingizio cha kulazimisha agenda zake" dhidi ya kisiwa hicho kinachotawaliwa kidemokrasia.