Waziri Mkuu wa New Zealand ashinda uchaguzi kwa kishindo

Waziri Mkuu Jacinda Ardern

Waziri Mkuu wa New Zealand Jacinda Ardern Jumamosi ameshinda uchaguzi mkuu kwa kishindo, kwa kupata ushindi wa waliowengi.

Wakati theluthi mbili ya kura zikiwa zimeh esabiwa, chama chake cha Labour cha mrengo wa kushoto kilikuwa tayari kimeshinda zaidi ya asilimia 49 ya kura na kinatarajiwa kupata kiasi ya viti 64 katika bunge la nchi hiyo lenye wabunge 120.

Idadi hiyo ni kubwa vya kutosha kwa kiongozi wa upinzani Judith Collins kukubali kushindwa na kumpigia simu Ardern kumpongeza.

“Hongera kwa mafanikio yako kwa sababu naamini ushindi huo ni mzuri kwa matokeo ya uchaguzi kwa chama cha Labour. Ilikuwa ni kampeni ngumu,” Collins amesema hayo akiwa mjini Auckland.

Chama chake cha National Party cha kiconservative kitachukua viti 35 katika kile kinachoonekana ni uchaguzi dhaifu kwao kutokea kwa takriban miaka 20.

Hakuna kiongozi wa kisiasa aliyeweza kupata viti vingi bungeni tangu New Zealand ilipoanzisha mfumo wa kura za uwiano mwaka 1996, na kupelekea kuwepo serikali kadhaa za mseto.

Matokeo ya uchaguzi kwa upande wa Ardern ni bora zaidi kuliko ilivyotegemewa na kunauwezekano wa kukipa chama cha Labour ushindi wenye nguvu mara nyingine tangu 1946.

Alikuwa amepongezwa sana kwa uongozi wake wakati wa janga la virusi vya corona, vilivyosababisha vifo 25 katika nchi yenye watu milioni 5.

Alionyesha hisia za masikitiko na kuchukua maamuzi katika udhibiti wa bunduki baada ya mzungu mbaguzi kuua Waislam 51 katika shambulizi msikitini mwaka 2019.

Ardern alionyesha uongozi imara katika kushughulikia maafa yaliyotokana na kulipuka kwa volcano katika kisiwa cha White Island, ambacho pia kinajulikana kama Whakaari, ambapo watu 21 walifariki na kuacha darzeni wamejeruhiwa Disemba mwaka 2019.