Wazazi wawasilisha DNA katika zoezi la kuwatafuta watoto waliouawa Uganda

Watu wa eneo hilo wakiwa wamekusanyika nje ya Shule ya Sekondari ya Mpondwe Lhubirira, tarehe 17 Juni 2023. Picha na REUTERS/Stringer.

Wazazi ambao bado hawajapata miili ya watoto wao kufuatia shambulio kwenye shule iliyopo magharibi mwa Uganda, walikusanyika katika kituo cha polisi cha mji ambao tukio lilitokea ili kuwasilisha sampuli za seli za nasaba, DNA ili kuitambua miili ya watoto wao kati ya maiti 42 zilizopatikana.

Mauaji hayo yalitokea Ijumaa usiku katika Shule ya Sekondari ya Lhubirira, ni moja ya mauaji ya kikatili yalitokea nchini humo katika miongo ya hivi karibuni. Washambuliaji walichoma moto bweni lililojaa wanafunzi wavulana, na baadaye kushambulia bweni lililojaa wasichana, na kuwauwa wanafunzi hao kwa kuwakatakata kwa mapanga na visu.

Katika tukio hilo pia, washambuliaji waliwateka nyara wanafunzi sita. Maafisa wa usalama wanasema washambuliaji ni wapiganaji wa kundi la Islamic State lenye makao yake upande wa pili wa mpaka wa Uganda katika misitu ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kamanda wa polisi wa mkoa huo, Tai Ramadhan alisema maiti nyingi zilichomwa moto kiasi cha kutoweza kutambulika, hivyo kuwalazimu wachunguzi kutumia sampuli za DNA kutoka kwa ndugu na jamaa ambao wanajaribu kuwatambua.

Simon Kule, alifika katika kituo cha polisi cha Bwera ili kutoa sampuli ya DNA, kwani anendelea kumtafuta mtoto wake, Philmon Mumbere.

Alisema "Kwa hivyo wanapaswa watusaidie ili tujue - kama watu hawa bado wapo au wako kwenye chumba cha kuhifadhia maiti ili tujiandae."

Nae Solomon Mulekya alikuwa akimtafuta binti yake, Trephine Kaghuo, alisema.

"Hatuna furaha, kwa sababu tumepoteza watoto wetu," alisema. "Ninawasiwasi, kama waasi wamemchukua na hatufahamu kama waliwaua njiani."

Maafisa walisema Jumatatu kuwa watu 20 wanaoshukiwa kuwa "washirika" waliofanya uvamizi huo, akiwemo mwalimu mkuu wa shule hiyo wanashikiliwa ili kuhojiwa.

Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la Ruters